Na. Elinipa Lupembe
Wananchi wa kata ya Bwawani na vitongoji vyake, wamejitokeza kwa wingi kuchangamkia huduma ya kupima afya bure, iliyotolewa kwenye Zahanati zao kwa siku tatu mfululizo, huduma iliyotolewa bure bila malipo yoyote.
Huduma hiyo ya vipimo na dawa imetolewa na halmashauri ya Arusha kwa ufadhili wa wadau wa afya kutoka Shirika la Project Abroad - Tanzania, ambapo watu wamepata fursa ya kupima afya zao na kupatiwa dawa mara baada ya ugonjwa kugundulika.
Wananchi hao, licha ya kushangazwa na huduma hiyo, ambayo haijawahi kutokea ndani ya kata yao, wamesema kuwa wamepata fursa ya kuchunguza afya zao kwa magonjwa mbalimbali ambayo hawakuwahi kufikiria kupima bila ya kuugua.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mungushi, mheshimiwa Jacob Toronge, amesema kuwa, kutokana kata hiyo kuwa pembezoni mwa mji, sio rahisi mtu kwenda hospitali kupima bila ya kuwa mgonjwa, kutokana na umbali wa eneo loa mpaka kufika hospitali.
Toronge ameongeza kuwa kituo cha Afya kipo Nduruma zaidi ya Kimita 15 huku hospitali ya mkoa ni zaidi ya Kilomita 30, hivyo sio rahisi sana mtu, kutoka Bwawani kwenda hospitalikupima bila kuugua.
"Tunaishi mbali sana na hospitali na vituo vya afya, mtu wa Bwawani ni vigumu kwenda hospitali bila kuugua, ni mpaka awe mgonjwa ndipo anaweza kwenda hospitali, lakini leo tumerahisishiwa kwa kuletewa huduma za vipimo nyumbani" amesema Mwenyekiti huyo.
Mchungaji Julius Loita, aliyefika kupima afya, kwenye moja ya zahanati kupata vipimo, amesema kuwa, huduma ya upimaji afya ni ya msingi kwa wananchi hasa, waishio maeneo ya pembezoni, kwa kuwa inawapa fursa kujua hali za afya zao.
Mkurugenzi wa mradi, shirika la Project Abroad Florence Mdodi, amesema kuwa shirika lao linajishughulisha na uchunguzi, wa hali ya afya kwa jamii, kwa kutoa fursa ya watu kupima magonjwa yasiyoambukiza na yanayoambukiza pamoja na kutoa dawa za magonjwa hayo.
Aidha Mdodi, amefafanua kuwa, lengo la kutoa huduma hiyo ni kuwataka watu kupima afya zao, hata kama hawajisikii kuumwa kitu chochote kutokana na ukweli kuwa, kuna baadhi ya magonjwa huchelewa kuonesha dalili.
"Ni utaratibu mzuri kwa mtu, kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kuepuka madhara ya kuachelewa kuanza matibabu" amesisitiza Mdodi.
Ameongeza kuwa, ugonjwa wowote ukigundukika mapema ni rahisi kutibika na mgonjwa kurudia afya yake haraka, tofauti na ugonjwa ukigundulika kwa kuchelewa mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Naye Muuguzi Mkuu, halmashauri ya Arusha sista Agusta Komba ameyataja magonjwa yaliyokuwa yanapimwa ni pamoja na ugonjwa wa macho, pressure, magonjwa ya mfumo wa hewa, maambukizi ya njia ya mkojo 'UTI', Vidonda vya tumbo na minyoo pamoja na HIV.
Hata hivyo, Muuguzi huyo amesema kuwa, watu waliogundulika na magonjwa walipatiwa ushauri nasaha pamoja na dawa na wale waliokutwa hawana ugonjwa wowote walipatiwa ushauri wa namna ya kuendelea kujikinga kupata magonjwa.
Ameongeza kuwa na baadhi ya wagonjwa, walipatiwa rufaa kwenda hospitali za wilaya na mkoa kwa matibabu na uchunguzi zaidi.
Aidha, Komba amesema kuwa zaidi ya wananchi mia nane, wamejitokeza na kupata huduma za vipimo na kupatiwa dawa huku akisisitiza kuwa huduma hiyo itakuwa inatolewa kila baada ya miezi minne kwenye, maeneo ya pembezoni ambako hakuna vituo vya afya vyenye maabara.
Huduma hiyo imetolewa kwenye zahanati za Themiyasimba, Mungushi, Bwawani pamoja na zahanati ya Kyoga kata Olturoto.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.