Na. Elinipa Lupembe.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na wazee, imezitaka shule zote Tanzania, kuanzisha Dawati maalumu la malalamiko ambalo watoto watapata fursa ya kutoa taarifa za ukatili watakaofanyiwa kwenye jamii zao.
Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya watoto, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Sebastian Kitiku, wakati wa mdahalo wa wanafunzi wa shule ya msingi Engalaoni kata Mwandeti, halmashauri ya Arusha, uliofanyika shuleni hapo.
Kitiku amesema kuwa, Dawati hilo maalumu, litajihusisha na kupokea malalamiko ya watoto wanaofanyiwa matukio ya ukatili na kuyashughulikia huku itoa fursa kwa watoto, kuchagua walimu watatu kwenye shule zao, walimu ambao, watoto wenyewe wataona ni walimu rafiki na wao watakua huru kuwaeleza hali yoyote ya ukatili au viashiria vya ukatili utakaofanyika dhidi yao.
Aidha Kitiku amefafanua kuwa, Dawati hilo ni mkakati endelevu wa Wizara, utakaoongeza mtandao wa watoto kutoa taarifa ya matukio ya ukatili katika kuendeleza na kurahisisha, mapambano dhidi ya ukatili wanaofanyiwa watoto.
Aidha ameongeza kuwa licha ya dawati hilo, Wizara imeongeza njia za kutoa taarifa kupitia simu ya bure kwa kupiga namba 116 na kutoa taarifa muda wowote.
"Namba 116 itatumika kutoa taarifa ya ukatili dhidi ya mtoto, mtoto mwenyewe anaruhusiwa kipiga simu na mtu yoyote atatumia namba hiyo kutoa taarifa za ukatili wa mtoto kwa muda wowote atakapokuwa ana taarifa yoyote ile". Amesema Kitiku.
Aidha, Wakati wa mdahalo huo, watoto wa shule ya msingi Engalaon, walionesha kusikitishwa na mila na desturi za jamii yao ya Kimaasai za kuwaozesha watoto wa kike wakiwa na umri mdogo huku wakilazimika kukatishwa masomo na ndoto zao za maisha.
Watoto hao wameongeza kuwa mila za kimasai, licha ya kandamizi kwa wanawake na watoto wa kike lakini pia upo ukatili kwa watoto wa kiume ambao huwazuia kwenda shule na badala yake kuachwa nyumbani wakichunga ng'ombe.
Hata hivyo watoto hao wamethibitisha wao wenyewe kuanza, kupambana na mila hizo kandamizi, kupitia klabu iliyoanzishwa shuleni hapo mwaka jana na shirika la WDCD baada ya kugundulika kuwa zaidi ya wasichana 70 shuleni hapo walikuwa wamechumbiwa, wakisubiri kuolewa.
Aidha watoto hao wamesema kuwa kupitia klabu hiyo, wamepata elimu juu ya haki zao na namna ya kukabiliana na mila hizo huku wakitoa taarifa pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili.
Naio Baraka mmoja wa wanafunzi aliyekuwa amechumbiwa, amesema kuwa baada ya kujifunza haki zake kupitia klabu ya watoto shuleni hapo, na taryari alikuwa amechumbiwa, aliweza kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na shule na baadae baba yake kulazimika kurudisha mahari, na sasa yupo shule anaendelea na masomo, akiwa mwenye matumaini makubwa ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mwalimu.
"Baba yangu alitaka kuzima ndoto yangu ya kuwa mwalimu, kwa kutaka kuniozesha kwa mwaname mzee, nikiwa na miaka 14, ninafurahi amerudisha mahari, sasa nitakuwa mwalimu na kuelimisha jamii". Amesema Naio.
Hata hivyo uongozi wa kijiji cha Engalaoni, unaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa jamii hiyo, kuachana na mila potofu huku jamii hiyo ikiendelea kubadilika.
Mwenyekiti wa Kamati ya shule ya msingi Engalaoni, Mzee Laizer amethibitisha kuwa kwa sasa jamii imeanza kuelimika na kutaka serikali kuwaelimisha taratibu kwa kuwa hizo ni mila ambazo walirithi kwa mababu zao, na hapo awali, hawakufahamu madhara yake.
"Jamii yetu haikufahamu kuwa mila hizi zina madhara makubwa kwa watoto, na sisi tumezirithi kutoka kwa mababu na mababu, hivyo naomba serikali iendelee kutuelimisha tuu, na wengi wameanza kuelewa sasa" amesema Laizer.
Hata hivyo, licha ya mapambano dhidi ya ukatili wa watoto, tafiti zinaonyesha bado hali ni mbaya, watoto wakike 3 kati ya 10 wanafanyiwa ukatili huku mtoto 1 wa kiume kati ya 10 anafanyiwa ukatili wa kingono, na asilimia 49 ya matukio hayo hufanyika nyumbani na ndugu wa familia, asilimia 23 hufanyika njiani na asilimia 15 hufanyika shuleni.
Mdahalo huo umefanyika kwa lengo la kusikiliza changamoto za watoto wakati wa kuelekea maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika mkoa wa Arusha, yatakayofanyika tarehe 13.06.2018 kwenye viwanja vya sheik Amri Abeid, Jijini Arusha yenye Kauli mbiu ya 'KUELEKEA UCHUMI WA VIWANJA, TUSIMUACHE MTOTO NYUMA'.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.