Na. Elinipa Lupembe.
Wilaya ya Arumeru imeanza kutumia teknolojia mpya ya kutumia nyuki kulinda vyanzo maji, mbinu ambayo imesaidia kupunguza shughuli za binadamu ndani ya misitu yenye vyanzo vya maji ikiwemo shuguli za kilimo na ufugaji zilizokuwa zikifanyika hapo awali na kuharibu mazingira hayo, licha ya kuwa ufugaju nyuki huo ni shughuli ya kuongeza kipato kwa wananchi.
Akitoa ufafanuzi kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019, wakati akikagua mradi wa Uhifadhi wa Msitu wa Jamii Lemanda, mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amesema, wamebaini kuwa pamoja na hatua zingine zinazochukuliwa kutunza mazingira hasa ya vyanzo vya maji ni wananchi wa maeneo hayo kuruhusiwa, kufuga nyuki ambao ni askari thabiti wa kupambana na binadamu waharibifu wa mazingira.
Naye Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 kitaifa, ndugu Mzee Mkongea Ali, amewataka viongozi na watendaji wa wilaya hiyo kutowaonea huruma wanaochezea vyanzo vya maji kwani ni sawa na kuchezea maisha ya watu.
Aidha amesisitiza kuwa licha ya sheria zilizowekwa za kutoza faini kwa atakaebainika kuharibu mazingira, ni vema kwa muhalifu huyo kuongezewa adhabu ya kufanyakazi ya kutunza mazingira kwa kusafisha na kumwagilia bustani, kwenye maeneo ya umma kama hospitali na vituo vya afya.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamesema uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji bado ni mkubwa hasa kwenye maeneo ya wafugaji, ambao huingiza mifugo ili kupata malisho, tatizo ambalo athari zake zinaonekana wazi na kwamba jitihada za ziada zinahitajika, licha ya Serikali kuwa na mipango mikakati mizuri.
Anton Mollel, mkazi wa kijiji cha Lemanda, amesema kuwa, bado kuna changamoto kubwa ya uelewa kwa jamii ya wafugaji, juu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira, kwa kuendelea kuingiza mifugo yao kwa ajili ya malisho kwenye maeneo ya vyanzo vya maji jambo ambalo , linahitaji juhudi za ziada kuwaelimisha wafugaji hao.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.