Na. Elinipa Lupembe.
Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini, halmashauri ya Arusha, mpango unaotekelezwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii - TASAF awamu ya III, wameanza mkakati wa kujipanga kuondokana na umasikini uliokithiri, uliokuwa ukizikabili kaya hizo, kuelekea kufikia ukomo wa mradi huo.
Mwandishi wa habari hizi, alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na vikundi vitano, vinavyotokana na wanufaika wa mpango huo wa kunusuru kaya masikini, katika kijiji cha Engorora kata ya Kisongo, wakati wa semina elekezi ya kuwajengea uwezo, wa kuboresha shughuli za kuweka na kuwekeza fedha kupitia kikundi.
Wanufaika hao, wamethibitisha kuwa, wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya kuweka na kuwekeza fedha, wanazopata kutokana na mpango na zile wanazopata kutokana na shughuli zao nyingine, kwa lengo la kuwa na fedha kwa ajili ya dharura na vipindi vigumu vya maisha, pamoja na kuanzisha shughuli mbalimbali za kuongeza kipato cha kaya zao.
Wamesema kuwa, licha ya serikali kupitia TASAF kuwapa fedha za ruzuku za mpango wa kunusuru kaya masikini, lakini pia imeweza kuwajengea uwezo wa kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa, vikundi ambavyo vimewawezesha kuanzisha shughuli mbalimbali za kuinua kipato, ikiwemo kilimo, mifugo na biashara ndogondogo.
Naitanamwang'aik Sambwete, Mwenyekiti wa kikundi cha Erereto, amesema kuwa, kwa sasa, wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini, wameanza kujiwekea mikakati ya kujikwamua kiuchumi, kupitia vikundi vyao vya kuweka na kukopa, vikundi ambavyo vinawapa fursa ya kukopeshana fedha na kupata mitaji ya kuanzisha shughuli mbalimbali za kibiashara.
Naitanamwang'aik ameeleza kuwa, kikundi chao kilianza mwaka jana, mwezi Juni, 2018 kikiwa na wanachama 15, kwa kuweka akiba ya shilingi 2,500 kila wiki, na kukopeshana kwa riba ya asilimia 5, na baada ya miezi 12, waliweza kugawana kiasi cha shilingi 182,500, kwa faida ya shilingi 62,500 kwa kila mwana kikundi.
Amethibitisha kuwa licha ya faida hiyo ya elfu 62 kwa mwaka, zaidi wanakikundi walipata fursa ya kukopa na kuanziasha shughuli za uzalishaji pamoja kutatua matatizo ya kifamilia ikiwemo matibabu, kulipa karo na kununua mahitaji ya familia zao.
Hata hivyo kikundi hicho kimeweka mkakati wa kuchanga shilingi 5,000 kila mwezi na kuanza kumnunulia mwanakikundi mmoja mbuzi wa maziwa, na wanategemea baada ya miezi 15, kila mwanakikundi atakua na mradi wa mbuzi wa maziwa, mradi ambao wanaamini utaongeza pato la familia.
Esuvat Levosu wa kikundi cha Upendo, ameshuhudia kuwa, tangu mradi huo wa TASAF, kuwajengea uwezo wa kuanzisha vikundi vya kuweka, kuwekeza na kukopeshana, wameweza kuzikwamua familia zao kiuchumi, tofauti na hapo awali, maisha ya familia zao yalikuwa magumu na yasiyokuwa na mwelekeo.
" Familia zetu zilikua na maisha ya kuunga unga, maisha ya kubahatisha na yasiyo na mwelekeo, kupitia vikundi vyetu, tunauhakika wa kuendesha maisha ya familia zetu, na tumeanza kuweka mikakati ya muda mrefu, hata mradi wa masikini ukiisha tutakuwa na shughuli za kutuingizia pesa" amesema Esuvati.
Katibu wa Kikundi cha Meseyeki, Febronia Buani, amesema kuwa, tangu tumeanza kuwa na kikundi cha kuwekeza na kukopeshana, ameweza koboresha mradi wake wa ng'ombe wa maziwa, kwa kukopa fedha zilizomsaidia kununua chakula bora cha mifugo yake na kumfanya kufuga kisasa zaidi, huku ng'ombe hao wakitoa maziwa mengi tofauti na hapo awali alikua alifuga kienyeji.
"Nilikuwa nafuga ng'ombe lakini sikuwa na uwezo wa kufuga kisasa, tangu nimejiunga kwenye kikundi cha kuweka na kuwekeza fedha,nimeweza kukopa na kuboresha mradi wangu wa ng'ombe wa maziwa, kwa kutumia fedha hizo kufuga kisasa, nanunua pumba, majani, virutubisho na kuwatibu ng'ombe wangu kwa wakati pindi wanapougua, ng'ombe ni wazuri na wameanza kutoa maziwa mengi zaidi kwa sasa" amethibitisha Fabiola
Aidha Fabiola ameongeza kuwa, wamekuwa wakishauriana shughuli za kufanya kama wanakikundi ili kuweza kujipatia kipato, pamoja na kufuatiliana kuhakikisha kila mwanakikundi ameanzisha au kuendeleza shughuli ya kuingiza kipato, huku wakifuatilia zaidi matumizi sahihi ya fedha ambazo mwanakikundi amekopa ili aweze kurejesha na kuepuka matumizi tofauti ya fedha hizo.
Awali, Mratibu wa TASAF mkoa wa Arusha, Mathias Seif, amefafanua kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha walengwa wote wa mpango wa kunusuru kaya masikini, ni kuwa na shughuli rasmi za kuwaingizia kipato, shughuli ambazo zitaimarisha uchumi wa kaya kwa wakati wote, hata mradi utakapofikia ukomo.
Ameongeza kuwa, TASAF imekuwa ikitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa vikundi hivyo, lengo likiwa kuwajengea uwezo wa kuweka akiba na kuwa na fedha za kutumia wakati wa vipindi vigumu, pamoja na kuwekeza fedha kwa ajili ya kukopeshana na kuanzisha shughuli endelevu za kuwaingizia kipato, ili kuondokana na umasikini uliokithiri kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2025.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.