AMLAKA ZA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI ZATAKIWA KUTUMIA FURSA ZILIZOPO KATIKA SHERIA YA PPP
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ametoa rai kwa Mamlaka za Serikali pamoja na wawekezaji kutoka Sekta binafsi kutumia fursa zilizopo katika Sheria ya Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ili kupata faida na kuipunguzia Serikali mzigo wa kibajeti.
Mhe. Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo Mjini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya, kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, sura Na. 410, Sheria ya Ubia kati ya sekta ya Umma na Binafsi, Sura Na. 103 na mafunzo ya matumizi ya takwimu zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma, uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
Aliwahimiza Maafisa Masuuli wote kuzingatia maelekezo ya Waraka wa Hazina namba 7 wa mwaka 2020/21 unaotoa maelekezo na mwongozo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa utaratibu wa PPP.
Alisema kuwa Sheria ya PPP Sura 103 imefanyiwa marekebisho kwa kuweka mazingira wezeshi ili kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, Sheria hiyo inaruhusu wawekezaji katika miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kunufaika na vivutio vya kikodi na visivyokuwa vya kikodi, sawa na wale wanaopata vivutio chini ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania, Sura ya 38.
“Sheria ya PPP inaruhusu taasisi za umma kununua mbia anayekidhi vigezo moja kwa moja kwa miradi isiyohitaji ushindani ili kupunguza muda wa hatua za ununuzi na pia imetoa fursa kwa wawekezaji wa kigeni kushirikisha wazawa katika miradi ya PPP ili kuwawezesha kiuchumi na kuendeleza wataalamu wa ndani”, alisema Dkt. Nchemba.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.