Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imezindua rasmi msimu wa ununuzi wa zao la Parachichi kwa mwaka 2025/2026 huku ikisisitiza udhibiti wa ubora na uongezaji thamani ili kuongeza mchango wa zao hilo katika pato la Taifa na kuinua kipato cha wananchi.
Uzinduzi huo umefanyika tarehe 25 Septemba 2025, mkoani Njombe, ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka ambaye amesisitiza umuhimu wa wakulima kuuza zao la Parachichi kwa wakati ili kuepuka hatari ya mazao kuharibika na kupoteza ubora. Aidha, amebainisha kuwa hatua hiyo itawasaidia wakulima kupata bei nzuri na yenye tija, sambamba na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya Kimataifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen J. Nindi amesema Serikali imejipanga kuimarisha mnyororo wa thamani wa Parachichi, kuendeleza masoko ya Kimataifa na kukuza kilimo cha biashara chenye tija kwa wakulima.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za uhifadhi, uongezaji thamani na utafiti, ili kuhakikisha Parachichi linalozalishwa Tanzania linaendelea kukidhi viwango vya Kimataifa. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ajira kwa vijana, kukuza ushindani wa bidhaa kwenye soko la Dunia na kuinua kipato cha wakulima mmoja mmoja.
Washiriki ambao ni pamoja na wakulima, wanunuzi, wasindikaji na wasafirishaji wa zao la Parachichi walipata fursa za kujadiliana namna bora ya kuendeleza Tasnia ya Parachichi, hususan katika kuongeza thamani, kuboresha ubora na kufungua fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Washiriki wengine walioshiriki ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bi Irene Mlolwa; Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uendelezaji wa Mazao ya Mbogamboga na Matunda (TAHA), Dkt. Jacqueline Mkindi; Wakuu wa Wilaya; na Wakurugenzi wa Halmashauri mbalimbali kutoka maeneo tofauti yanayolima zao la Parachichi nchini.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.