Na Elinipa Lupembe
Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2023, kuna mafanikio ya uelewa wa jamii katika suala zima la Ulinzi na Usalama wa mtoto ambao unaongezeka siku hadi siku.
Akizungumza ofisini kwake na mwandishi wetu, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, halmashauri hiyo, Stedvant Kileo, amesema kwamba, licha ya changamoto za matukio ya ukatili dhidi ya watoto nchini, amefafanua kuwa, halmashauri ya Arusha kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali imefanikiwa kuanzisha Kamati za Ulinzi na Usalama wa mtoto ngazi ya kata na Wilaya (MTAKUWWA), kamati zinazofanya kazi ya kuelimsha na kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa Ulinzi na Usalama wa mtoto kwa kuzingatia haki za mtoto zilizoanishwa na Umoja wa Mataifa na Mataifa ya Afika.
Aidha halmashauri imeweza kuanzisha klabu za kupinga ukatili kwa watoto shule za msingi na sekondari, klabu ambazo zinawapa fursa watoto wenyewe kujitambua, kutambua haki zao, kuyafahamu matukio ya ukatili pamoja na kujilinda dhidi ya ukatili sambamba na kutoa taarifa ya matukio ya kikatili dhidi yao.
"Tuna klabu 100 kwa shule za msingi na klabu 35 kwa shule za sekondari pamoja na madawati ya kijinsia kwa shule zote, kwa pamoja zikiongozwa na walimu wa malezi wanaojengewa uwezo wa ulinzi na usalama wa mtoto mara kwa mara". Amefafanua Kileo.
Aidha halmashauri inashirikiana na taasisi za serikali ambazo ni wajumbe wa MTAKUWWA ngazi za kata na wilaya wakiwemo Jeshi la Polisi, Polisi kata, Dawati la kijinsia la Polisi, Maafisa Magereza, Maafisa Uhamiaji, wazee wa mila, viongozi wa dini pamoja na Mahakimu na weaendesha mashitaka wanaoushughulikia kesi za watoto kwa ufasaha na haraka.
Kupitia majukwaa hayo, jamii imeanza kuelimika na kuripoti matukio ya ukatili wanayofanyiwa watoto ndani ya jamii ikiwemo, ubakaji, ulawiti, ndoa za utotoni pamoja na watoto kutumikishwa jambo ambalo limewezesha watuhumiwa kukamwatwa na baadhi kutiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo jela.
Hata hivyo amewataka wazazi na walezi wanaowapa watoto wao simu, kufuatilia maudhui wanayoyaangalia na kupakua kupitia simu hizo, kwa kuwa kupitia simu hizo, watoto wanajifunza maadili mabaya ambayo ni kinyume na mila na desturi za kitanzania.
"Kufuatia Kauli Mbiu ya mwaka huu inamtaka mzazi na mlezi kuzingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa Kidigitali, hivyo ni jukumu la wazazi na walezi kuwasimamia watoto juu ya matumizi ya simu janja na mitandao ya kijamii, kompyuta pamoja na televisheni" Ameongeza Mkuu huyo wa Idara.
Kwa upande wake muendesha mashitaka Koplo Jane Mandu, kituo cha Polisi Ngaramtoni amesema kuwa kuanzia mwezi Januari mpaka Juni jumla ya matukio 23 yaliripotiwa huku kesi 8 zikitolewa hukumu, kesi 6 watuhumiwa wakihukumiwa kifungo cha maisha na kesi 2 wakihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Koplo Jane amesema kuwa licha ya jamii kuanza kuripoti matukio ya ukatili dhidi ya watoto, bado kuna changamoto ya wanajamii kushindwa kujitokeza kutoa ushahidi mahakamani kwa kuhofia kuharibu mahusiano yao na watuhumwa, kwa kuwa matukio mengi ya ukatili yanatokea nyumbani yakihusiha ndugu, jamaa na marafiki.
"Jeshi la polisi kwa kushirikiana na raia wema, wanajitahidi kufuatilia watuhumiwa wa matukio ya ukatili dhidi ya watoto lakini bado kuna baadhi ya mashahidi kutoka ndani ya jamii, kushindwa kutoa ushahidi jambo ambalo linasababisha baadhi ya watoto kukosa haki zao, pindi kesi zinapowasilishwa kwenye vyombo vya sheria". Amefafanua Koplo Jane.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.