ARUSHA DC YAPAA KIMAPATO.
Halmashauri ya Arusha imepaa katika ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi billioni 4.8 mpaka billioni 6.9 kwa mwaka ikiwa ni hatua kubwa ya mafanikio katika ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato vinavyomilikiwa Halmashauri.
Wakizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024-2025 waheshimiwa Madiwani kwa ujumla wamempongeza Mkurugenzi ndugu Seleman Msumi pamoja na Wataalamu wake kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuwataka kuongeza juhudi zaidi katika kubuni vyanzo vipya vya mapato ili Halmashauri iweze kukusanyaji zaidi na kuchochea kasi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine Baraza hilo pia limetoa pongezi kwa Halmashauri ya Arusha kwa kuanzisha zoezi la upimaji wa maeneo ikiwa ni mpango wa kukabiliana na migogoro ya ardhi ambapo Mkoa wa Arusha ni moja katika ya Mikoa yenye changamoto hiyo katika jamii.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi, ndugu Stedvant Kileo amewahakikishia waheshimiwa Madiwani kuwa ofisi ya Mkurugenzi kwa kushirikiana na Wataalam wa Halmashauri hiyo wataongeza juhudi katika kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato, ukusanyaji na usimamizi wa fedha zinazotokana na vyanzo mbalimbali.
"Pamoja na pongezi hizi tulizo zipokea kutoka kwa waheshimiwa Madiwani bado tunahitaji kuongeza juhudi kwenye maeneo yetu ya masoko ikiwemo kuongeza nguvu kazi Ili kuhakikisha hakuna mapato yanapotea Ili Halmashauri yetu iweze kuharakisha maendeleo kwa kupitia mapato yetu ya ndani". Alisema Kileo.
Sambamba na hayo,pia Kikao hicho cha Baraza kimeiagiza Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha Wataalam wanaisimamia ipasavyo miradi yote inayoanzishwa Ili kuchochea maendeleo ya wananchi na ukusanyaji wa mapato ndani ya Halmashauri.
Kikao hicho cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Arusha kimefanyika leo tarehe 05/11/2024 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Dkt.Ojung'u Salekwa kikiwa ni kikao cha kwanza cha robo ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.