Na. Elinipa Lupembe.
Mashirika yasiyo ya kiserikali, yanayofanya shughuli zake ndani ya halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru, yameridhishwa na utaratibu uliowekwa na serikali wa kufanya kazi pamoja, lengo likiwa ni kusaidia wananchi kupambana na maadui njaa, umasikini na maradhi kwa ajili ya maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na wadau hao wa Maendeleo, wakati wa mkutano wa kuwasilisha na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Asasi hizo, kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2020, mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Arusha.
Wadau hao wa Asasi za kiraia, wamesema kuwa, kufanya kazi na Serikali kumewesha Asasi hizo, kufanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za serikali, kwa kuzingatia viapumbele na malengo ya serikali, pamoja na Asasi hizo kufanya tathmini ya kazi zilizofanyika kwa kila robo ya mwaka.
Wadau hao wameridhishwa na utaratibu uliyowekwa na Serikali ya Awamu ya tano, wa kuwasilisha taarifa za utekeleza za Asasi hizo, kila baada ya miezi mitatu, lengo likiwa kufanya tathmini ya kazi zilizofanyika, na kupanga mikakati ya kazi, inayoendana na malengo ya serikali kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa.
Mkurugenzi wa shirika la BIGLGEO, Edward Kang'oma, amesema kuwa, Asasi za kiraia zimeridhishishwa na utaratibu uliowekwa na serikali ya awamu ya tano, utaratibu unaonesha wazi kuwa, serikali inatambua na kuthamini kazi zinazofanywa na wadau hao, na kuongeza kuwa kuweka wazi taarifa za shughuli za Asas hizo, zinaongeza ufanisi katika kazi pamoja na kuondoa ufisadi na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya Asasi.
" Tunaridhishwa na utaratibu uliowekwa na serikali yetu makini, utaratibu huu unatuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi kulingana na vipaumbele vya serikali, kufanyakazi kwa uwazi, kujitathmini katika kazi pamoja na kuibua miradi kulingana na mahitaji wa jamii katika maeneo husika". Amesema mkurugenzi Kang'oma
Hata hivyo, Msajili Msaidizi wa Mashirika yasiyo ya serikali 'NGOs', halmashauri ya Arusha, Ahadi Mlai, amesema kuwa lengo la serikali ni kuunganisha nguvu za pamoja kati ya mashirika na serikali ili kuhakikisha malengo na vipaumbele vya serikali vinafikiwa kwa pamoja.
Aidha Msajili huyo, amezitaka Asasi hizo, licha ya kutekeleza miradi kulingana na vipaumbele vya serikali, lakini utekelezaji wa kazi zao ulingangane na maandiko ya miradi yao, jamii ifahamu miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, pamoja na kuwasilisha kwa mkurugenzi wa halmashauri, taarifa za utekelezaji wa shughuli hizo kwa kila robo ya mwaka.
"Asasi za kiraia zinatakiwa kushirikisha jamii miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, kuwajibika kwa jamii wanayoihudumia kwa kuweka wazi taarifa za mradi na gharama za mradi pamoja na kazi zinazofanyika kila robo ya mwaka" amesisitiza Msajili huyo Msaidizi.
Jumla ya Asasi 25 zinazofanya kazi ndani ya halmashauri ya Arusha, zimetekeleza agizo la Serikali za kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli zinazotekelezwa na ASAS hizo kwa kipindi cha robo ya pili kwa mwaka 2020.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.