Na Elinipa Lupembe
Shirika lisilo la kiserikali la Center for Women and Children Develepment (CWCD) limezindua mradi wa kuwatetea watoto wa kiume, kwa kuanzisha klabu za wavulana kwenye shule za msingi 6, unaojulikana kwa jina la Maabara ya watoto wa kiume shuleni 'BOY'S VAC LAB'.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, mkurugenzi wa shirika la CWCD, Hindu Mwego, amesema kuwa, shirika limekuja na mradi wa kuwawezesha watoto wa kiume kujitambua na kutambua haki zao kama ilivyo kwa watoto wa kike,, kutokana na ukweli kwamba, watoto wa kike wamekuwa wakitetewa na kuwaacha nyuma watoto wa kiume ambapo madhara yake yameanza kujitokeza sasa kwenye jamii.
Ameongeza kuwa, Takwimu za Jeshi la Polisi za mwaka 2021, zinaonyesha kati ya matukio ya ukatili 391 yaliyoripotiwa, matukio 312 ni matukio ya ulawiti kwa watoto wa kiume, huku takwimu zikishuka kwa watoto wa kike hali iliyolisukuma shirika kuanza programu ya kuwahudumia watoto wa kiume.
"Kwa takwimu hizi, ni dhahiri kuwa jamii imejikita kuwatetea watoto wa kike huku watoto wa kiume wakiachwa nyuma, jambo ambalo linasababisha watoto wa kiume kufanyiwa vitendo vya ukatili huku jamii ikiona kuwa watoto hao wana uwezo wa kujitegemea, jambo ambalo sio sawa, watoto wa kiume nao wanapaswa uangalizi na kutetewa kama ilivyo kwa watoto wa kike". Amesisitiza mama Hindu
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Selemani Msumi licha ya kulishukuru shirika hilo, amethibitisha uwepo wa ongezeko la matukio ya ulawiti kwa watoto wa kiume, huku jamii ikijikita zaidi kumlinda mtoto wa kike.
Ameongeza kuwa, kwa sasa jamii inalazimika kuanza mkakati wa kuwatetea watoto wote, kwa kuwa hata watoto wa kiume wana haki ya kulindwa kama ilivyo kwa watoto wa kike.
"Tumeanza kuona matokea ya kuwatetea na kuwalinda watoto wa kike peke yake, na kuwaacha watoto wa kiume wakijitegemea kimakuzi, na matokeo yake yameanza kujitokeza, kwa sasa tunashuhudia makundi ya vijana wadogo wakijiingiza kwenye vitendo vya uhalifu, kama ilivyo kwa vijana wanaojiita panya road ambapo hivi karibuni wamekuwa wakijeruhi watu, kupora Mali zao na hata kuua watu wasio na hatia". Amefafanua Msumi
Hata hivyo watoto walioshiriki mafunzo hayo, wamefurahishwa na mradi huo, kwa kuweka wazi kuwa ni kweli watoto wa kiume wamekuwa wakiachwa nyuma, hivyo kuanza mkakati wa kuwalinda na kuwatetea wavulana utaleta matunda mema kwa jamii.
Simplisit Siprian, mwanafunzi wa darasa la (5) shule ya msingi Ngaramtoni, amesema kuwa kuna umuhimu wa kuwatunza na kuwatetea watoto wa kiume, kwa kuwa nao wanahitaji kulindwa kama ilivyokuwa watoto wa kike.
"Watoto wa kiume wasiachwe nyuma, wapewe haki sawa na watoto wa kike, kushindwa kufanya hili kunasababisha wavulana kujiingiza kwenye makundi ya kiuhalifu kwenye jamii, vijana wavulana ndio wanapora na kuiba mali za watu pamoja na kuua watu mitaani". Amefafanua mwanafunzi Simplisiti.
Naye Mratibu wa Dawati la Jinsia na mpelelezi wa kesi za ukatili, kituo cha Polisi Ngaramtoni, Koplo Jane Kitundumandi, amethibitisha uwepo wa matukio ya ukatili kwa watoto na ulawiti kwa watoto wa kiume katika jamii yetu, na kuitaka jamii kutoa ushirikiano wa kuwa wakweli na wawazi katika kutoa ushahidi ili kuwatetea watoto na kuhakikisha wanapata haki zao dhidi ya ukatili wanaofanyiwa.
"Changamoto kubwa inayokwamisha kesi za ukatili dhidi ya watoto ni mila na desturi za kimaasai, kwa kufanya vikao vya usuluhishi kwenye familia zao nyumbani, usuluhishi unaokwamisha ushahidi na watoto wengi kupoteza haki zao, lakini kwa sasa tutatumia nguvu hata kwa mashahidi ili kufanikisha kesi hizo". Amefafanua Koplo Jane
Shirika la CWCD, linafanya kazi za kijamii ndani ya halmashauri ya Arusha kwa kutoa huduma za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye kata 19 za halmashauri hiyo huku mradi wa 'Boy's Vac Lab' ukitekelewa kwenye shule 6 za msingi za Moivo, Naurei, Olturoto, Ilboru, Kiranyi na Ngaramtoni. kwa ufadhili wa shirika la Foundation For Civil Society.
ARAUHA DC
KaziIendelee✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.