Na Elinipa Lupembe
Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's) halmashauri ya Arusha yametakiwa kufanya kazi kwa kufuata taratibu na kuzingatia vigezo na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa, kushindwa kufanya hivyo mashirika hayo yatachukuliwa hatufa za kisheria ikiwemo kungiwa kutoa huduma katika wilaya hiyo.
Hayo yamewekwa wazi na mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashirika (NGO's), uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano halmashauri ya Arusha, na kuwasisitiza kufanya kazi kwa kufuata taratibu.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasisitiza mashirika hayo kuibua miradi kwa kuzingatia changamoto za jamii na kuitekeleza miradi hiyo kama iliyoanishwa kwenye maandiko ya mradi na si vinginevyo huku akiwata kutekeleza miradi yenye tija kwa jamii.
Amesema kuwa sheria ziko wazi kila shirika linatakiwa kuishirikisha serikali shughuli zote zinazofanyika kuanzia ngazi ya wilaya halmashauri, kata, vijiji na vitongoji na kuwasilisha taarifa hizo kila robo ya mwaka kwa mkurugenzi kupitia msajili wa mashirika wilaya.
"Nisisitize mashirika yote yanayofanyakazi kwenye wilaya yetu, kuhakikisha mnafanyakazi kwa kushirikisha serikali kwa ngazi zote, ni utekelezaji wa majukumu yenu kufanya miradi yenye tija kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa, hatutasita kusitisha kazi za NGO ambayo inayotekeleza miradi isiyo na tija kwa jamii yetu" Amesisitiza mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya ameyapongeza mashirika hayo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kushirikiana na serikali kuhudumia jamii ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi kiseka.
" Kazi yenu ni bora sana, serikali inatambua na kuthamini sana kazi za mashirika, jambo la msingi ni kufuata sheria na taratibu bila kuathiri maadili ya watanzania na Taifa kwa ujumla, fanyeni miradi yenye tija kwa nchi yetu na si vinginevyo" Amesema Mhe. Emmanuela.
Naye Msajili Msaidizi wa NGO's halmashauri ya Arusha, Ahadi Mlai amesema sheria na taratibu za kuendesha mashirika ziko wazi, licha ya kushirikisha serikali kwa ngazi zote, ila shirika linatakiwa kufanya kazi kwa uwazi kwa kuhakikisha jamii yote inafahamu mradi unaotekelezwa na manufaa yake katika maeneo wanayotekeleza mradi.
"Kabla ya kutekeleza mradi lazima waombe kibali kwa serikali, kwa kuonyesha gharama za mradi, muda wa utekelezaji, eneo la utekelezaji na umuhimu wa mradi huo kwa jamii, kutangaza mradi kwa jamii husika ili kila mwanajamii afahamu kinachoendelea katika eneo lao" Amefafanua Mratibu huyo.
Zaidi ya NGO's 40 zimesajiliwa kufanya kazi katika Halmashauri ya Arusha, yakiwa yamejikita katika kuhudumia jamii kwenye sekta za afya, kilimo na mifugo, ujasiriamali, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii.
Awali mashirika yasiyoya kiserikali yamekutana na kufanya mkutano wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli zao kwa kipindi cha mwaka uliyopita wa 2022, mkutano ambao unafanyika kwa mujibu wa sheria, zinazoyasimamia mashirika hayo nchini.
ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.