Na. Elinipa Lupembe.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango, amekabidhiwa rasmi jengo la vyumba vitatu vya madarasa, meza na viti 150, vyenye thamani ya shilingi milioni 60, katika shule ya sekondari Mateves, halmashauri ya Arusha, mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo, kufuatia agizo la mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kukamilisha ujenzi huo ifikapo tarehe 15.12.2021.
Akipokea jengo hilo, mkuu huyo wa wilaya, amewapongeza wasimamizi na watekelezaji wote wa mradi huo, kuanzia ngazi ya halmashauri, kata, shule kamati ya ujenzi pamoja na mafundi wazalendo, kwa kuwezesha kukamilisha ujenzi huo kwa wakati na zaidi jengo hilo likiwa kwenye viwango vya ubora, vinavyoakisi thamani ya pesa zilizotumika.
Mhandisi Ruyango amekwenda mbali zaidi kwa kuishukuru Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu, kwa kuboresha miundombinu ya shule, licha ya kuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, kubwa zaidi utekelezaji wa mpango wa mapambano dhidi ya UVIKO 19, kwa walimu na wanafunzi wawapo darasani.
"Shilingi bilioni 2 tulizopokea za ni fedha nyingi sana, tusingeweza kuzipata kwa kuchangisha kwa wananchi, ninamshukuru na kumpongeza sana Rais wetu, amefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya Elimu kwa muda mfupi, haijawahi kutokea, watoto wetu watasoma kwa raha lakini na wananchi nao wamepunguziwa mzigo wa michango ya ujenzi wa madarasa mwaka huu" amesisitiza Mkuu huyo wa wilaya.
Naye mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, ameweka wazi kuwa, halmashauri inaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba 100 vya madarasa na samani zake, ikiwa ni madarasa 96 kwa shule 30 za sekondari na madarasa 4 kwa shule 2 za msingi shikizi, huku baadhi ya madarasa yakiwa tayari yamekamilika, na maendeleo ya mradi mzima ukiwa umefikia zaidi ya 90% za ukamilishaji.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti halmasahuri ya Arusha na Diwani wa kata ya Mateves, ambapo ujenzi katika shule ya kata yake umekamilika na kukabidhiwa, Mhe. Freddy Mollel, licha ya kuipongeza serikali, ameweka wazi kuwa, wananchi wamepata matumaini makubwa sana na serikali yao, kwa kuwa wana uhakika watoto wao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2022, wataanza masomo yao kwa wakati, huku wakishukuru kwa kupumzishwa na michango ya ujenzi wa madarasa kwa mwaka huu.
"Niseme tuu, tunaendelea kuishukuru na kuipongeza serikali ya awamu ya sita, kwa kutujengea madarasa ya kidato cha kwanza, kwa idadi ya wanafaunzi 300, waliopangiwa shuleni hapa, kama si fedha hizi, tungekuwa na hali ngumu sana, kiukweli wananchi wamepumzika na michango, michango ambayo ilikuwa ni mzigo kwao katika maeneo mengi"amefafanua Makamu huyo Mwenyekiti.
Awali, Mkuu wa shule ya sekondari, Mateves, Mwalimu Sayuni Tarimo, ameishukuru serikali kwa kuwapatia idadi hiyo ya madarasa, na kuahidi kuwasimamia wanafunzi kuyatunza madarasa hayo pamoja na samani zake kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo huku wakifundisha kwa bidii na kupandisha kiwango cha taaluma sambamba na mapambano dhidi ya UVIKO 19.
ARUSHA DC
KaziInaendelea✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.