Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango amewaagiza wataalamu wa afya wa halmashauri ya Arusha kufanya maandalizi mapema ili kuweza kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ambao hivi karibuni mlipuko wake umetokea katika nchi jirani ya Uganda.
Mhandisi Ruyango ametoa maagizo hayo wakati wa kikao cha kamati ya afya ya msingi halmashauri ya Arusha kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo ambapo kimejumuisha viongozi wa dini na mila pamoja na wadau mbalimbali ili waweze kuwa mabalozi wa kutoa elimu hiyo waliyoipata katika maeneo wanapofanyia shughuli zao.
Aidha amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa changamoto kama vile upungufu wa rasilimali, dawa, vifaa tiba na kinga, ni muhimu kufanya maandalizi mapema na kuiandaa timu maalum ya ufuatiliaji pamoja kuelimisha Umma juu ya hatari ya ugonjwa huu na namna ya kujikinga.
.“Tukumbuke ugonjwa huu hauna tiba bali kinga na unaenea kwa haraka hivyo sisi kama Halmashauri ni vyema kuchukua tahadhari mapema ikiwemo kufanya ukaguzi wa afya kwa wageni wanaoingia nchini hasa katika mipaka isiyo rasmi na kuandaa vituo maalumu kwaajili ya kufanya vipimo vya ugonjwa huo”. Alisisitiza Mhandisi Ruyango.
Naye Mjumbe wa kamati ya Afya halmashauri ya Arusha Dkt. Japhet Champanda wakati akiwasilisha taarifa ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo amesema kuwa, Kila mwananchi anawajibika kuchukua tahadhari za kujikinga na kuwakinga wengine juu ya ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kuepuka kugusa wanyama kama vile popo, nyani, sokwe, tumbili na swala au mizoga ya Wanyama pamoja na kuzingatia usafi wa mazingira na usafi binafsi.
Hata hivyo wajumbe waliohudhuria kikao hicho wameipongeza halmashauri ya Arusha kwa niaba ya Serikali kwa hatua walizokwisha kuzichukua za kukabiliana na ugonjwa huo huku wakishauri elimu iendelee kutolewa katika mikusanyiko ya watu kama vile mikusanyiko ya kimila, makanisani, misikitini, mashuleni na minadani ili wananchi wapate elimu hiyo na wajue namna ya kujikinga.
"Ni vyema kila mtu kwa Imani yake amlilie Mungu ili aweze kutuepusha na janga hili huku elimu ikiendelea kutolewa bila kuleta taharuki kwa jamii ili kila mtu apate uelewa juu ya ugonjwa huu wa Ebola”. Alisistiza Mchungaji Pivs Edward Stevan, wa Kanisa la Naioth Gosple Assembly.
Mganga Mkuu Halmashauri ya Arusha Dkt. Petro Mboya ameweka wazi kuwa Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Arusha wametenga kituo cha afya Moshono kwa ajili ya kufanya matibabu ya wagonjwa waliogundulika na ugonjwa huo pamoja na eneo la TPRI kwaajili ya kuwatenga wahisiwa na waliokuwa karibu na wagonjwa wa Ebola.
Ifahamike kuwa ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na Kirusi aina ya Ebola chenye anuwai sita uligundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1976 katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan na dalili za ugonjwa huo ni kama vile kupata homa kali ya ghafla, maumivu ya kichwa, Maumivu ya mwili, misuli na viungo, Kuharisha kunakoweza kuambatana na damu, Kutapika damu, Vipele mwilini, Kuvia damu chini ya ngozi au kutokwa na damu puani , mdomoni , machoni na masikioni.
JIKINGE NA UGONJWA WA EBOLA, WAKINHE NA WENGINE
ARUSHA DC
KaziIendlee✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.