Na Elinipa Lupembe
Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's), halmashauri ya Arusha, yametakiwa kutekeleza miradi inayozingatia mahitaji ya jamii husika kwa kujikita katika kutekeleza vipaumbele vya serikali huku yakizingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa mashirika nchini.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango, wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli zilizofanywa na Mashirika hayo kwa kipindi cha robo ya kwanza, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano halmashauri ya Arusha.
Mkuu huyo wa wilaya licha ya kuridhishwa na taarifa za utekelezaji zilizowasilishwa na mashirika hayo, ameyasisitiza mashirika hayo, kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na vipaumbele vya serikali kisekta.
"Nimeridhishwa na kazi zinazofanyika, kwa kuwa zimejikita kutatua changamoto za jamii kwenye sekta ya elimu, afya, kilimo, lishe, biashara na ujasiriamali, uhifadhi na utunzaji wa mazingira, kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, lakini zaidi napongeza suala la kupambana na mmea hatari wa gugu karoti". Amebainisha Mhandisi Ruyango.
Aidha ameyaagiza mashirika hayo kuandaa mikakati ya kuanza kutoa elimu kwa makundi ya viongozi ili kuwajengea uwezo wa kuwa na maadili ya uongozi ili kuwa na viongozi wanaozingatia mustakabali mzima wa utawala bora kwa jamii.
Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya ameweka wazi kuwa, serikali inatambua na kuthamini kazi zinazofanywa na mashirika hayo, ikiwa ni utekelezaji wa malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi, kazi ambazo zilipaswa kufanywa na serikali.
Nao wawakilishi wa mashirika hayo wameishukuru serikali kwa kuyaamini mashirika na kushirikiana nayo katika kutoa huduma za jamii kwa niaba ya serikali zaidi wakimpongeza mheshimwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuthamini kazi zinazofanywa na ASAS za kiraia huku akiisisitiza serikali kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika.
Herieth Raju mwakikishi wa shirika la GLAMI ameishukuru halmashauri kwa ushirikiano na amewataka wadau wanaofanya kazi zinazofanana, kushirikiana na kufanyakazi kama timu pamoja na kubadilishana uzoefu kwa kuweka mikakati ya kuhudumia jamii kwa pamoja ikiwa ni kuhamasisha na kuwajengea wananchi uwezo wa kujitegemea.
"Kwa mfano Mashirika yanayosupport wanafunzi kupata chakula shuleni, wawajengee uwezo wazazi wa kutambua kuchangia chakula cha watoto wao shuleni ni jukumu lao, badala ya kuwapa chakula cha bure kwa miaka yote, jambo linalowafanya baadhi ya wazazi kubweteka na kuona kama hilo si jukumu lao". Amesema Herieth
Naye Msajili wa Mashirika halmashauri ya Arusha Ahadi Mlay, ameyapongeza mashirika hayo kwa ushirikiano sambamba na uwasilishaji wa taarifa za robo kwa wakati na kuwasisitiza, kuhakikisha wanatekeleza shughuli zao kama maandiko ya miradi yao yanavyoelekeza na si vinginevyo.
Awali kikao hicho ni kikao cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kipindi cha Julai - Septemba 2022 ni cha kawaida kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya serikali za mitaa, inayoyataka mashirika yasiyo ya kiserikali, kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli zinazofanyika kwa kila robo ya mwaka huku jumla ya mashirika 30 kati ya 38 yamewasilisha taarifa zake.
ARUSHA DC
KaziInaendelea ✍✍✍.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.