Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda amewatoa hofu wananchi wa wilaya hiyo kuwa, hakuna mtu aliyepoteza maisha kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia tarehe 23. 03.2023, mvua iliyosababisha uharibifu wa mali na makazi ya watu kwa baadhi ya maeneo ya Tarafa ya Mukulat.
Mhe. Kaganda ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake eneo la Usa-River, kufuatia uvumi uliosababisha taharuki kwa baadhi ya watu, ukisemekana kuwa, mvua hiyo ilisababisha vifo vya watatu waliokuwa wamepanda pikipiki moja baada ya kupatikana pikipiki hiyo ikiwa imefunikwa kwenye kifusi cha matope, eneo la kibaoni Ngaramtoni.
"Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Jeshi la polisi, umebaini hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha kufuatia mvua hivyo tuzipuuze taarifa hizo kwa kuwa hazina ukweli wowote". Amefafanua Mkuu huyo wa wilaya.
Ameongeza kuwa, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za kusadikika kuwa kuna watu waliokiwa wamepanda pikipiki, hawakujulikana walipo na Jeshi hilo kufanya uchunguzi wa awali na kumpata mmiliki halali wa pikipiki akiwasilisha kadi ya umiliki iliyoripotiwa kituo cha polisi cha Usa River na mtu huyo kuthibitisha kuwa walikuwa wanaume wawili na mwanamke mmoja kwenye pikipiki hiyo ambapo wanaume hao walipambana na kujiokoa wenyewe huku mwanamke akiokolewa na wasamaria wema usiku huo.
Aidha, kulingana na tathimini iliyofanywa na wataalamu wakati wakitembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko, wamegundua, uwepo wa uchafuzi wa mazingira hasa utupaji wa taka ngumu ambazo zinasababisha mitaro kuziba na kushindwa kupitisha maji wakati wa mvua, uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji ikiwemo ukataji wa miti holela zikiwa ni sababu za maji kukosa uelekeo pindi mvua zinaponyesha.
Hata hivyo, amewataka wananchi wa wilaya ya Arumeru kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ikiwa ni pamoja na kuhama kwenye maeneo ya mkondo wa maji, kujenga majengo imara kwa kutumia tofali ngumu ili kuepuka kuta kuanguka wakati wa mvua nyingi pamoja na kuhifadhi taka ngumu wenye maeneo yaliyoainishwa.
Vile vile, Mhe. Kaganda ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau mbalimbali kujitokeza kutoa msaada wa kibinadamu kwa wananchi waliokumbwa na athari za mvua hiyo kubwa kwa kuchangia chakula, mavazi na malazi kupitia ofisi ya Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha.
Awali, mvua hiyo kubwa ilisababisha uharibifu wa mali za wanachi katika kata zilizo Oltrumet, Oloirien, Sambasha, Olmotonyi na kata ya Kimnyaki.
ARUMERU YETU
KaziInaendelea✍✍✍
Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhe.Emannuela Mtatifikolo Kaganda, akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake mapema jana.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.