Kaimu mkuu wa wilaya ya Arumeru na Mkuu wa wilaya ya Monduli Mhe, Idd Kimanta amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuzuia wananchi kulipia huduma za maji na badala yake kujikita zaidi, kuwaelimisha umuhimu wa kulipia huduma hiyo.
Kaimu mkuu huyo wa wilaya amesema hayo wakati wa akinduzi rasmi bodi mpya ya Mamlaka ya Maji Ngaramtoni 'NGAUWSA' baada ya wajumbe wake kuteuliwa na waziri mwenye dhamana wa ofisi ya Rais TAMISEMI.
Mheshimiwa Kimanta ameeleza kuwa kuna baadhi ya viongozi ambao huwashawishi wananchi kukataa kulipia huduma ya maji kwa madai kuwa, huduma hiyo inagharamiwa na serikali jambo ambalo si la kweli.
Amefafanua kuwa, ifike wakati viongozi kuacha siasa kwenye suala la maji na kuwataka viongozi kuwahamasisha wananchi wao, kujua umuhimu na faida za kulipia huduma za maji na si kuwadanganya na kuwapoteza wakatae kulipia maji.
" Nina uzoefu kuna baadhi ya viongozi wanawaambia wananchi wasilipe maji, viongozi, waelezeni wananchi ukweli, huduma ya maji inalipiwa na hakuna maji ya bure! Hivi bomba likiharibika litatengenezwa na nani?" Amehoji Kimanta.
Aidha Kimanta amefafanua kuwa huduma ya maji ni lazima ilipiwe, na ipo kisheria, ili miradi ya maji iweze kujiendesha na wananchi kuwa na uhakika wa kupata huduma hiyo kila siku.
Hata hivyo amewataka wananchi kutambua kuwa kazi ya serikali ni kujenga miundo mbinu ya maji na kuhakikisha huduma imewafikia wananchi lakini kuiendeleza miradi hiyo ni jukumu la wananchi kwa kulipia huduma hiyo.
"Fedha amabazo wananchi wanalipia maji hutumika kukarabati miundo mbinu ya maji, kulipa wahudumu pamoja na kuongeza uwanda wa upatikanaji wa maji kwa watu wasiokuwa na maji" amesema Kimanta.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha mheshimiwa Noah Lembris amesisitiza kuwa suala lolote la maendeleo ya wananchi halihitaji siasa, viongozi kwa kushirikiana na wananchi wanatakiwa kujitoa katika shughuli za maendeleo bila kujali tofauti zao za kiitikadi.
Na kuongeza kuwa wanatambua Bodi ya maji ipo kisheria, jambo la muhimu ni kuwapa ushirikiano wajumbe wa bodi hiyo ili kuhakikisha wananchi wa Ngaramtoni wanapata huduma ya maji safi na salama na si vinginevyo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.