Na. Elinipa Lupembe.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha, Selemani Msumi ameitaka jamii, kuhudumia watoto wenye uhitaji katika maeneo yao, kwa kufanya hivyo kunawapa watoto hao faraja na zaidi inasaidia watoto hao kufikia malengo na ndoto zao.
Mkurugenzi Msumi ameyasema hayo ofisini kwake, wakati akiwakabidhi msaada watoto wenye uhitaji, kata ya Kiutu, msaada ambao umewezeshwa na halmashauri kwa kushirikinana na wasamaria wema pamoja na wadau wa maendeleo halmashauri ya Arusha.
Msumi amesisitiza kuwa, licha ya serikali kuwa na mpango na mikakati ya kusaidia watoto hao, kupitia programu ya mpango wa kunusuru kaya masikini lakini bado haijaweza kufanikiwa kuwafikia watoto wote, kulingana na idadi kubwa ya watoto wenye uhitaji nchini, na kuongeza kuwa jamii inahitajika kujitoa kwa hali na mali, kusaidia watoto hao, ndani ya jamii zao.
"Tunawafahamu watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, watoto wenye uhitaji tunaishi nao, niwasihi wanajamii kujitoa kusaidia watoto wenye hao kwenye maeneo yetu, jambo ambalo linasisitizwa hata kwenye imani za dini zetu , kiimani wanasema, 'nyumba inayohudumia watoto wenye uhitaji inawaka taa mbele za Mungu' na 'nyumba isiyohudumia wenye uhitaji, taa imezimika' tuwe taa inayowaka ni baraka mbele za Mungu pia" amesisitiza Mkurugenzi huyo.
Aidha Mkurugenzi Msumi amewashukuru wadau na wasamaria wema waliojitoa, kutoa msaada huo kwa watoto wenye uhitaji, na kuwataka wadau wengine kujitokeza kusaidia watoto hao, kwani hilo ni jukumu la wanajamii wote.
Afisa Ustawi wa Jamii, Halmasahuri ya Arusha, Beatrice Tengi, amesema kuwa, halmashauri kwa kushirikiana na shirika la Huruma Ophanage na msamaria mwema, wametoa msaada wa vyakula, sabuni, madaftari na kalamu kwa watoto 50 wa kata za Kiutu, Mwandeti, Bwawani, Bangata na Oljoro.
Amefafanua kuwa watoto hao 50 wamegawiwa mchele Kilo 5, maharage Kilo 3, sabuni ya unga mche 1, na pakiti 1 ya sabuni ya unga, madaftari 4 na kalamu kwa kila mmoja na baadhi yao wamepatiwa nguo kulingana na uhitaji.
Halmashauri ya Arusha inawakaribisha wadau wa maendleeo na wasamaria wema, kuendelea kujitoa kwa hali na mali kutoa msaads kwa watoto wahitaji, walio kwenye vituo maalumu na wale wanaoishi ndani ya jamii.
ARUSHA DC
KaziInaendelea✍✍✍✍
PICHA ZA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.