Na. Elinipa Lupembe.
Wakuu wa shule za sekondari halmashuri ya Arusha, wametakiwa kuacha kufanyakazi kwa mazoea badala yake, kubadili mitazamo kwa kubuni mbinu mpya na kutumia teknolojia za kisasa kufanya kazi ili kupandisha kiwango cha taaluma kwenye shule wanazozisimamia.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule, alipokutana na wakuu hao wa shule kwa mara ya kwanza na kufungua, mkutano wa robo ya nne wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania 'TAHOSSA' ngazi ya Wilaya, halmashauri ya Arusha, mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa chama cha walimu mkoa wa Arusha - CWT.
Mkurugenzi Mtambule, amewataka wakuu hao wa shule, kuwa wabunifu kwa kusoma na kujifunza mbinu mpya kupitia mitandao na kuzitumia mbinu hizo katika ufundishaji, kupanga mikakati mipya, itakayomuwezesha mwanafunzi kujifunza kwa urahisi na kuwafanya wafanye vizuri katika masomo yao.
"Mnatakiwa kuwa wabunifu katika kutekeleza jukumu lenu la kufundisha, msifundishe kwa mazoea, msifanye kazi kwa mazoea 'bussiness as ussual' haifai, bali tumieni muda mwingi kujifunza teknolojia mpya za kufundishia, hii itawarahisishia ufundishaji na wanafunzi kujifunza pamoja na kupandisha kiwango cha taaluma na hatimaye ufaulu kuongezeka "amesisitiza Mkurugenzi Mtambule
Aidha amewataka Wakuu hao wa shule, kuwaunganisha walimu na watumishi wasio walimu wanaowaongoza kwenye taasisi zao, kufanya kazi kama timu na kuwalea kwa upendo ili kuondoa migogoro baina yao na kuwafanya waipende kazi hali ambayo inawezesha maisha ya amani kazini na kuongeza juhudi kazini, jambo ambalo litaongeza pia ufaulu kwa wananfunzi kwenye shule.
Hata hivyo wakuu hao wa shule, wamekiri kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na mkurugenzi huyo, ikiwa ni pamoja na kujenga upendo baina yao na walimu wanaowaongoza na kuahidi kushirikiana nae kwa hali na mali katika kutekeleza majukumu yao kwa maendeleo ya wanafunzi wanao wafundisha, shule zao na halmashauri kwa ujumla.
Mkuu wa shule ya sekondari Mwandet mwalimu Joseph Masawe, licha ya kumshukuru mkurugenzi huyo kwa kuanza kutatua kero za walimu kwa kipindi kifupi alichokaa katika halmashauri hiyo, amemuahidi kwa niaba ya wakuu hao wa shule kuwa, hawatamuangusha, wako tayari kufanya mabadiliko ya kiufundi katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na suala zima la ufundishaji na malezi, wakiwa na lengo la kupandisha kiwango cha taaluma kwa wanafunzi na kupandisha ufaulu wa shule katika halmashauri hiyo.
Hata hivyo Katibu wa Chama cha walimu, wilaya ya Arumeru, mwalimu Salome Gwandu, amewasisitiza wakuu hao wa shule kuwasimamia walimu wanaowaongoza, kutimiza wajibu wao kwa kuwawezesha kutekeleza majukumu yako kwa amani na upendo bila upendeleo wala ubaguzi kati yao, bali kuwajibika kama kanuni za chama cha Walimu zinavyoelekeza kuwa ni Haki na Wajibu.
"CWT inasisitiza kuwa hakuna haki bila wajibu, licha ya changamoto za kiutumishi zinazowakabilia walimu, mna wajibu wa kuhakikisha mnawezesha walimu kutimiza wajibu wenu kwa kutekeleza majukumu yenu ya kazi kama yanavyoelekezwa na mwajiri, CWT inawajibika kumtetea mwalimu aliyetimiza wajibu wake na sio vinginevyo" ameweka wazi katibu huyo.
Mkutano huo wa robo ya nne wa Umoja wa Wakuu wa shule Tanzania (Tanzania Heads Of Secondary School Association - TAHOSSA), umejumuisha wakuu wa shule za sekondari 56 za halmashauri ya Arusha ikiwa shule 32 za serikali na shule 24 za binafsi.
Wakuu wa shule za sekondari halmashauri ya Arusha wakiwa kwenye mkutano wa robo ya nne wa Umoja wa Wakuu wa shule za sekondari Tanzania ngazi ya wilaya - TAHOSSA
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Saad Mtambule akizungumza na Wakuu wa shule za sekondari halmashauri ya Arusha wakati akifungua mkutano wa robo ya nne wa Umoja wa Wakuu wa shule za sekondari Tanzania ngazi ya wilaya - TAHOSSA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.