Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema viongozi na vyombo vingine havifanyi kazi ipasavyo kwenye Wilaya kitu ambacho kinasababisha ukuwepo na ubadhirifu wa fedha za umma.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo Septemba 16, 2023, wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Majaliwa wilayani Tandahimba, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi Mkoani Mtwara.
Kauli ya Dkt.Samia ilikuja baada ya taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa, ambaye amesema katika wilaya hiyo zimetolewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya lakini ujenzi huo bado haujakamilika.
Aidha, Dkt. Samia ameshangazwa na viongozi mbalimbali ngazi za wilaya na halmashauri pamoja na kamati za siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa kusimamia udhibiti wa matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.
“Kamati za siasa ziko wapi, wakuu wa wilaya wako wapo, madiwani wapo, kwanini fedha itumike vibaya, lakini jengine, watu wa TAKUKURU kwenye wilaya hii wako wapi, kazi yao ni kuzuia na kupambana wasisubiri kupambana, kuzuia matumizi mabaya lakini kuzuia Rushwa.”
“Kwahiyo sielewi kwanini hali ifike hivi wakati viongozi wote wa serikali maeneo yote wako hapa.” DKT. Samia.
Ikumbukwe Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alipofanya ziara wilayani humo Agosti 13, 2023 alitoa maagizo kwa TAKUKURU kuchunguza matumizi ya fedha shilingi Bilioni 1.5 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa vituo Vitatu vya afya ambavyo ujenzi wake bado haujakamilika.
Vituo hivyo ni kituo cha afya cha kata ya Mambamba, kituo cha afya kata ya Mihambwe na kituo cha afya kata ya Litehu.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.