Na Elinipa Lupembe
Katibu mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dr. John Jingu amezipongeza Taasisi za SOS Children’s Tanzania na Turkish Maarif Schools kwa ubunifu na ushirikiano mkubwa na Serikali katika kuwalea, kuwatunza na kuwapa nafasi za masomo watoto yatima na wanaotoka kwenye mazingira magumu.
Dr. Jingu ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea Taasisi hizo zinazotoa huduma za watoto mkoani Arusha na kufanya mazungumzo na Taasisi hizo ili kujiridhisha na huduma zinazotolewa kama zinaendana na matakwa ya Serikali.
Aidha, ameusisitiza uongozi wa Taasisi hizo kuendelea kushirikiana na Serikali licha ya kuwa watoto hao ni yatima na wanatoka kwenye mazingira magumu, wanapatiwa malezi bora yanayoendana na maadili ya jamii za Kitanzania na kuongeza kuwa, ikiwezekana huduma zao zitolewe nchi nzima kwa kuwa zitasaidia kupunguza baadhi ya changamoto wanazopitia watoto wa aina hiyo nchini.
“Nimefurahi kuona mnawapa watoto wetu malezi bora kulingana na mila, desturi na tamaduni za Kitanzania, msingefanya hizi ‘intervention’ pengine watoto wangekuwa wanahangaika na kuzurura mitaani bila kuwa na mwelekeo lakini hapa mnawatunza kama familia zao, ubunifu mlioufanya ni jambo la kuigwa, mnachokifanya hapa Arusha, pangeni namna ya kueneza program hii nchi nzima”. Amesema Katibu Mkuu huyo.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi zingine zinazoendesha huduma kama hizo kuhakikisha kwamba zinafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ili kuwa na uhakika na huduma wanazozitoa na kuendelea kuwasaidia watoto wa Kitanzania wenye mahitaji kama hayo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la SOS Tanzania, David Mulongo kwa niaba ya Taasisi hizo, ameishukuru Serikali kupitia Wizara husika, kwa ushirikiano wanaowapa huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika hatua zote za uanzishwaji wa program mpya za kuwasaidia watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Shirika la SOS Children’s Center, lililopo eneo la Ngaramtoni, halmashauri ya Arusha, linajishughulisha na kuwasaidia wototo yatima na wanatoka kwenye mazingira magumu.
ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA ZIARA HIYO
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.