Na Elinipa Lupembe
Katika kuimarisha harakati za kupinga ukatili kwa wasichana, Shirika la DSW limejenga Kituo Salama cha Wasichana kijiji cha Imbibya kata ya Mwandet, halmashauri ya Arusha lengo likiwa ni kuwapa eneo wasichana la kuweza kukaa na kubadilishana uzoefu, kujifunza stadi za maisha katika kasuala mbalimbali ya vijana.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, mkurugenzi wa shirika la DSW, Peter Owaga, amesema kuwa, kupitia mradi wa Binti na Maendeleo (BIMA), shirika limekuwa likifanya shughuli mbalimbali na wasichana, na hatimaye kuamua kuwajengea eneo la kudumu la kukutania na kupata mafunzo kwa uhuru, utulivu na kwa mapana zaidi.
Jengo hili litatumika kama darasa na maktaba ya kutoa mafunzo kwa wasichana na vijana, ambapo wasichana wa rika balehe watakutanishwa na watalamu wa kada tofauti na kuwapa elimu ya stadi za maisha, kujitambua na kukabiliana na ukatili wa kijinsia, Afya ya uzazi kwa vijana, uongozi, ujasiriamali na namna ya kujikwamua kiuchumi.
"Kituo kitawapa fursa vijana ya kukaa pamoja na kubadilishana uzoefu masuala ya ujana na ukatili, lakini zaidi kuwakutanisha na watalamu watakaowaelimisha namna ya kukabiliana na changamoto za ujana ikiwemo ukatili na elimu ya ujasiriamali" . Amefafanua Mkurugenzi Mbego.
Naye mgeni rasmi na Afisa Maendeleo Mkoa wa Arusha, Erena Materu, licha ya kulishukuru shirika hilo kwa kushiriki kutekeleza malengo ya Serikali kwa kuwekeza nguvu zaidi kwenye vipaumbele vyake, na kuwataka wananchi wa Imbibya hususani vijana kutumia kituo hicho ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
"Vijana wa Imbibya mna bahati san, halmashauri ina vijiji vingi lakini kituo kimejengwa kwenu, kazi kwenu kutumia kituo hicho na watalamu watakao kuwepo, mkikitumia vizuri na kuleta matokeo mazuri, na vijiji vingine vitajengewa vituo hivi, tunawategemea mkawe mfano wa vijana wa 'Arusha DC' na mkoa mzima wa Arusha." Amebainisha Erena
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha, Afisa Maendeleo ya Jamii - Dawati la Jinsia, Rovil Nguyaine, ameahidi kukisimamia kituo hicho kiweze kuwa endelevu hata pale mradi wa shirika utakapofika mwisho kwa kuhakikisha watalamu wanafika kituoni hapo kutoa huduma huku akiwasisitiza vijana kuhakikisha wanatumia kituo hicho ipasavyo.
Hata hivyo wananchi wa kijiji hicho, wamelishukuru shirika na halmashauri kwa kuhakikisha wanajenga kituo hicho, huku wakithibitisha, kupitia mradi wa Binti na Maendeleo, jamii imeanza kupata uelewa wa madhara ya ukatili wa kijinsia na kuanza kuachana na mila na desturi potofu.
"Kupitia mradi wa Binti na Maendeleo, jamii ya Imbibya imeanza kubadilika, kwa sasa ndoa za utotoni zimepungua, wasichana tunaendelea na masomo, hali ya ukeketaji imeanza kupungua licha ya kuwa bado kuna baadhi ya watu wanafanya kwa siri ila taratibu itafika mwisho" Amefafanua Glory Eliaman, mnufaika wa mradi wa BIMA
Awali DSW imetekeleza mradi wa Binti na Maendeleo kuanzia mwaka 2019 na utakamilika mwishoni mwa mwaka huu 2022, na kufanikiwa kujenga vituo salama kwa wasichana 2 na kuwafikia vijana 4,560, huku wadau 197 wakinufaika kupata elimu kwa ajili ya kwenda kuelimisha na kuhamasisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.
ARUSHA DC
KaziInaendelea✍✍
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA UZINDUZI WA KITUO SALAMA CHA WASICHANA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.