Kufuatia agizo la serikali la kuunda mabaraza ya wazee katika halmashuri zote, halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru imetekeleza agizo hilo kwa kukamilisha mchakato wa kuunda mabaraza hayo na hatimye kumpata mwenyekiti wa Baraza la wazee ngazi ya Halmashuri, katika uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Viongozi wa Baraza la wazee kutoka kwenye kata zote, zinazounda Halmashauri ya Arusha Wilayani Arumeru, wamefanya uchaguzi wa viongozi watakaounda baraza hilo, katika ngazi ya Wilaya pamoja na wajumbe watakao wawakilisha katika baraza la Madiwani.
Akizungumza wakati akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Kaimu Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Eliasifiwe Kileo, amemtangaza ndugu Elias Ngungat wa kata ya Olmotony, kuwa Mwenyekiti wa Baraza la wazee katika halmashuri ya Arusha, baada ya kupata kura 18 kati ya kura 50 zilizopigwa na kuwashinda wapinzani wake wanne waliogombea nafasi hiyo na kugawana kura 32 zilizosalia.
Aidha Kaimu Mwanasheria huyo, amewatangaza viongozi wengine watakaongoza baraza hilio ni pamoja na ndugu Aloyce Mollel kuwa Makamu Mwenyekiti, Julius Maras kuwa Katibu, na Florah Mollel kuwa Katibu msaidizi na mtunza Fedha ndugu Emaculata Lwali, baada ya wote hao kuchaguliwa na kushinda kwenye uchaguzi huo.
Aidha Eliasifiwe amewataja wajumbe wawili wawakilishi ‘ME’ na ‘KE’ ambaye ni ndugu Yohana Mengarana na Rose Laizer, watakaowawakilisha Baraza la Wazee wa Halmashauri hiyo kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani pamoja na kwenye mkutano wa Kamati ya kudumu ya UKIMWI.
Awali kabla ya uchaguzi huo kufanyika, Afisa Ustawi wa Jamii kitengo cha Wazee na Walemavu, Beatrice Tengi aliwaelezea Wazee hao, lengo uchaguzi huo ni kupata viongozi, watakao wawakilisha wazee wenzao kwenye ngazi ya wilaya, mkoa na hatimaye taifa.
Aidha Beatrice aliwataka wazee kuwachagua viongozi makini, watakaoweza kuwasilisha kero zao pamoja na kutetea maslai ya wazee ili kuhakikisha kila mzee anapata haki sawa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Arusha, Mganga Mkuu wa halmashauri Dkt. Peter Mboya, licha ya kuwapongeza viongozi waliochagulia, amewataka kuwawakilisha vema wazee wenzao waliowaamini na kuwapa dhamana kwa kuzitendea haki nafasi walizopewa ipasavyo pamoja na kuhakikisha wazee wanapata haki zao za msingi.
“ Ushindi mlioupata ni dhamana, mnatakiwa kuitendea haki nafasi hizo, kwa kuwatetea wazee wenzenu kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na ustawi wa wazee wa taifa hili, tekelezeni majukumu yenu ipasavyo kwa namna mtakavyoelekezwa na kitengo cha Ustawi ya Jamii ” amesisitiza Dkt. Mboya
Daktari Mboya, amewathibitishia wazee hao kuwa, halmashauri ya Arusha, imeandaa mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za wazee ikiwemo huduma muhimu ya afya kwa kuweka madirisha maalumu ya matibabu kwa wazee, kwenye hospitali na vituo vya afya.
Naye Mwenyekiti aliyechaguliwa, ndugu Elias Ngungat, amewashukuru wazee wenzake kwa kumwamini na kumpa dhamana ya kuwaongoza huku akiahidi kutumia uwezo alionao kuhakikisha anatetea haki za wazee wote bila kujali itikadi.
Aidha mwenyekiti huyo, ameishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kwa kuthamini kundi la wazee ambalo hapo awali kundi hilo lilikuwa halipewi kipaumbele.
Wajumbe wa Baraza la Wazee ngazi ya halmashauri, limaundwa na wajumbe watatu kutoka kila kata na kufanya Baraza la wazee halmashauri ya Arusha kuwa na jumla ya wajumbe 81 kutoka kata 27 za halmashauri hiyo.
PICHA ZA MATUKIO YA MKUTANO WA KUCHAGUA VIONGOZI.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.