Na.Elinipa Lupembe.
Jamii halmashaiuri ya Arusha, imetakiwa kuachana na mila na desturi potofu dhidi ya watoto wa kike, badala yake kuungana kwa pamoja, kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto, utakaowezesha mapambambano dhidi ya mimba za utotoni, mimba ambazo kimsingi zinazima ndoto za watoto wa kike kwa asilimia kubwa.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Viti Maalum Taifa, Mheshimiwa Amina Mollel, wakati akizungumza wakati wa Mkutano wa robo ya nne wa Baraza la Madiwani wa kuwasilidha taarifa za kata za halmashauri ya Arusha, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Amina, ametoa wito huo mara baada ya kuwasilishwa changamoto za ukatili kwa watoto wa kike hususani mimba za utotoni kwa baadhi ya kata, huku ikionekana mila na desturi bado ni tishio la utatuzi na udhibiti wa tatizo hilo.
Amefafanua kuwa, viongozi na jamii wanapaswa kufahamu kuwa, jukumu la kupambana na ndoa na mimba za utotoni, si la serikali peke yake, kazi ya serikali ni kuandaa sera rafiki, lakini jamii ndio watekelezaji wa sera hizo, hivyo ni jukumu la viongozi hao, kuungana kuelimisha jamii, kufahamu athari kubwa za mimba za utotoni kiafya, kisaikolojia, kiuchumi na kimtazamo pia.
Amewata madiwani hayo, jambo hilo kuwa agenda ya kudumu kwenye vikao vyao, kuanzia ngazi ya familia, kitongoji, vijiji, kata na hata wanapopata nafasi ya kuhudhuria kwenye vikao vya mila, kwa kuwashirikisha viongozi wa mila kupambana na ukatili dhidi ya watoto wa kike ikiwemo ndoa na mimba na ndoa za utotoni.
" Kila mnapokaa kwenye vikao vyenu, zungumzieni tatizo na athari za ndoa na mimba za utotoni, washirikisheni viongozi wa mila, umuhimu wa mtoto wa kike kupata elimu, hata mimi nisingepata fursa ya kusoma, nisingekuwa mbunge, palilieni ndoto za watoto wa kike na sio kuzikatisha" amesema mbunge Amina kwa hisia kubwa.
Naya Afisa Elimu Msingi, halmashauri ya Arusha, Hossein Mghewa, amesema kuwa, licha serikali kuweka sheria kali lakini changamoto kubwa bado lipo ndani ya jamii yenyewe, changamoto inayotokana na mila na desturi inayolazimisha usiri wa kutokutoa ushirikiano kwenye mapambano dhidi ya ukatili wa mtoto wa kike.
Hata kama serikali inapambana kuwapata wahalifu hao, jamii imekua ikiwaficha watuhumia wa kesi hizo, kwa kukubaliana kumaliza kesi nyumbani, huku wengine wakiacha kufika mahakamini kutoa ushahidi hata kama aliyefanyiwa ukatili huo ni mtoto wake wa kumzaa, jambo ambalo linaharibu mwenendo wa kesi hizo kufika mwisho ili mahakama iweze kutoa haki ya mtoto.
" Hata zikifanyika juhudi za kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani, kesi hushindwa kufika mwisho, familia nzima haifiki mahakamani kutoa ushahidi,hukutana na kumalizana wenyewe kimila, na wakati mwingine wazazi wenyewe, huwatorosha watoto" amesema Hossein
Hata hivyo bado serikali inaendelea kupanua wigo wa kuelimisha jamii hizo, kwa kuweka mikakati ya kupata wasaa wa kuzungumza na watoto na wazazi kupitia Idara ya Uthibiti Ubora wa shule, wakati wa ukaguzi wa shule ili kupata taarifa za siri kutoka kwao.
Mthibiti Ubora wa shule Fatuma Lema amethibitisha kuwa, kimeongezwa kipengele cha ukaguzi wa hali ya watoto shuleni hususani, mimba na ndoa za utotoni kwenye ukaguzi, kipengele kinachowalazimu kuzungumza na walimu , wanafunzi na wazazi, kwa lengo la kuelimisha na kutokomeza tatizo hilo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.