Na Elinipa Lupembe
Jamii imetakiwa kuwahasisha kina mama wajawazito halmashauri ya Arusha kuzingatia umezaji wa vidonge vya Madini Chuma na Folic acid,wanavyopewa kipindi cha chini ya wiki 12 za ujauzito pindi wanapohudhuria kliniki kwa wakati.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Tarafa ya Mukulat Hudhaifa Rashid kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Arumeru ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe wilaya, kwenye kikao cha tathmini ya Lishe kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Arusha.
Mwenyekiti huyo ametoa rai hiyo, kufuatia taarifa ya Afya ya Uzazi na Mtoto, iliyobainisha kuwepo kwa vifo vya watoto wakati wa kujifungua vinavyosababishwa na ulemavu wa mgongo wazi na tumbo nje, unaosababishwa ukosefu virutubisho, unaotokana na wajawazito kutokuzingatia kumeza vidonge vya Folic acid na madini chuma.
Ameitaka jamii kuwahamasisha wajawazito kuzingatia kuhudhuria kliniki kwa wakati na kuwakumbusha umezaji wa vidonge vyote wanavyopewa kwa kuwa ni muhimu katika hatua zote za ukuaji wa mwili wa mtoto akiwa tumboni na kushindwa kumeza vidonge hivyo kunaongeza hatari ya kumpoteza mtoto wakati wa kujifungua.
"Licha ya kwamba serikali inapambana kukabiliana na vifo vya watoto wakati wa kujifungua, bado kuna vifo vinavyotokana na uzembe wa wajawazito wenyewe, jambo ambalo si zuri sana kwa jamii na Taifa kwa ujumla, kunao uwezekano wa kuzuia vifo hivyo kama jamii na wajawazito wataamua" Amefafanua Rashid
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto, Sista Bujiku Butolwa, amesema kuwa 38% ya wajawazito huchelewa kuanza kliniki na kukosa kupata vidonge vya Folic Acid na madini chuma, vidonge ambavyo, mama mjamzito anatakiwa kumeza chini ya wiki 12 za ujauzito jambo linalosababisha watoto kuzaliwa wakiwa na ulemavu wa hali ya juu, unayosababisha vifo.
Hata hivyo Bujiku ameweka wazi, umuhimu wa vidonge vya Folic acid kwa wajawazito chini ya wiki 12 kuwa, ina Vitamin B9 inajumuisha dutu mbili zinazosaidia afya ya mwili, utengenezwaji wa seli hai nyekundu za damu, utengenezaji na ukarabati DNA na RNA ambazo ni dutu muhimu za jeni, husaidia mgawanyiko wa haraka wa seli hai katika mchakato wa ukuaji pamoja na kuimarisha afya ya ubongo, hususani kwa ukuaji wa mtoto aliye tumboni.
Naye Afisa Lishe halmashauri ya Arusha, Dotto Milembe ameweka wazi kuwa, vidonge vya Folic Acid sio dawa bali ni tiba lishe ambayo imetengenezwa maalumu kwa ajili ya wajawazito kutokana na hali ya wajawazito wengi kushindwa kula baadhi ya vyakula hivyo vidonge vya Folic acid na madini chuma, vimetengenezwa kama mbadala wa virutubisho vinavyotokana na aina nyingi ya vyakula.
"Vidonge vya Folic Acid na madini chuma, ni mbadala ya virutubisho vya aina nyingi vyenye umuhimu mkubwa katika hatua zote za kujenga mwili na akili ya mtoto kwa kuzingatia hatua zote ukuaji wa mtoto akiwa tumboni" Amefafanua Doto
Kikao cha tathmini ya Lishe, kwa kipindi cha robo ya tatu mwaka wa fedha 2022/2023 na hufanyika kila robo ya mwaka wa fedha, lengo likiwa ni kufanya ufuatilia wa watoto wenye utapiamlo kuanzia mama mjamzito, mtoto akiwa tumboni, kipindi cha kuzaliwa, watoto wa miaka 0 - 5, kinamama wanaonyonyesha, wanafunzi pamoja na jamii kwa ujumla wake.
"ARUSHA DC Ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
#KaziIendelee
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.