Na. Elinipa Lupembe.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa Chama cha Mapinduzi, wilaya ya Arumeru, wamefanya ziara na kukagua jumla ya miradi nane ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri ya Arusha kufuatia utekelezaji wa Ilani ya Chama ya mwaka 2015 katika halmashauri hiyo.
Katika ziara hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Arumeru, ndugu Simon Ole Saning'o, wamekagua miradi yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 12.5, katika sekta za Elimu, Afya, Maji na miundombinu ya barabara.
Wajumbe hao wa Kamati ya Siasa, wameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo, baada ya kubaini ubora wa miradi hiyo kwa kulinganisha na thamani ya fedha zilizotumika' value for mone', huku wakiwapongeza wananchi wa halmashauri ya Arusha kwa kujitoa kwa hali na mali kuchangia utekezaji wa maendeleo katika vijiji na kata zao.
Aidha Mwenyekiti Saning'o amesema kuwa, kati ya miradi nane iliyotembelewa miradi miwili ya ujenzi ya vyumba vinne vya madarasa na ofisi ya walimu shule ya sekondari Kiranyi na vyumba vitatu vya madarasa shule ya sekondari Lengijave, unatekelezwa kwa juhudi za wananchi mpaka kukamilika huku miradi mingine miwili wananchi wameichangia pia licha ya kupata fedha kutoka serikalini na wafadhili.
"Niwapongeze wananchi wa halmashauri ya Arusha, kwa kutambua umuhimu wa kutekeleza maendeleo kwenye maeneo yenu kwa faida yenu na vizazi vyenu, juhudi hizo zinaonyesha uwezo wa taifa letu kuanza kujitengemea na kuacha kutegemea misaada kutoka nje" amesema Saning'o
Hata hivyo Mwenyekiti Saning'o amesema kuwa licha ya asilimia kubwa ya miradi kutekelezeka kwa wakati, Kamati hiyo imebaini changamoto ya ucheleweshwaji wa ukamilishaji wa miradi ya maji ya vijiji kumi, iliyokuwa ikifadhiliwa na Benki ya Dunia, miradi ambayo mpaka sasa haijakamilika na kuitaka serikali kukamilisha miradi ili wananchi waweze kupata maji.
Naye Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Arusha, Angela Mvaa amethibitisha kuwa miradi hiyi ya maji ilianza mwaka 2013 na kusimama kwa muda mrefu, lakini kwa sasa Serikali ya awamu ya tano imeanza kutoa pesa kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi hiyo licha ya changamoto nyingi za mabadiliko ya kimazingira na tabia nchi kukabili utekelezaji wa miradi hiyo.
Hata hivyo Mvaa ameongeza kuwlicha ya changamoto za kuchelewa kwa miradi hiyo, mpaka sasa jumla ya miradi ya vijiji vitani kati ya kumi imekwishakamilika na tayari wananchibwameanza kupata maji, huku miradi ya vijiji vingine vitano ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Aidha Kaimu Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa, miradi yote ilikaguliwa na Kamati hiyo ya Siasa imetekelezwa na fedha kutoka Serikali Kuu, fedha za mapato ya ndani, kwa kushirikiana na wadau wa mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na nguvu za wananchi kwa usimamizi thabiti wa watalamu wa halmashauri hiyo kisekta.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umekwenda sambamba na ahadi ya mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, alipoingia madarakani kufuatia Ilani ya chama kinachoongoza serikali Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Mvaa ameitaja miradi iliyotembelewa na Kamati hiyo ya Siasa, ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Manyire, mradi wa ujenzi wa maktaba na ukarabati wa bwalo la chakula shule ya sekondari Mlangarini, ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na ofisi shule mpya ya sekondari Manyire.
Ujenzi wa madaraja Laroi na Mirongoine, ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa shule ya sekondari Kiranyi, ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya sekondari Lengijave, mradi wa maji wa vijiji vitano maarufu kama WaterAid, mradi wa maji Loovilukuny na mradi wa kivuko Matevesi.
Halmashauri ya Arusha inawataka wananchi kuendelea kuiamini na kuiunga mkono Serikali yao kwa kuchangia maendeleo katika maeneo yao, huku wakijikita katika kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo, kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2025.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.