Na Elinipa Lupembe
Kila mwanajamii ametakiwa kushiriki kikamilifu kupambana na kuzuia ukatili wa kingono kwa watoto wa kiume na wa kike,unaoendelea ndani ya familia na jamii zetu, ukatili ambao unasababiha athari kubwa kwa jamii, ili kuijenga jamii bora yenye haki na usawa.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Seleman Msumi, wakati wa kikao cha mwaka cha wadau wa kupinga Ukatili wa kingono kilichoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Center for Women, Children and Youth Development (CWCD) kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Msumi amesema kuwa, jamii inatakiwa kuwa karibu na watoto wao ili kuwapa elimu itakayobadilisha fikra na maisha yao hata watakapokuwa wakubwa.
“Wazazi wamekuwa ‘bize’ sana na shughuli zingine za Maisha na kusahau majukumu yao kama wazazi ya kuwalea watoto katika njia sahihi ya makuzi na malezi ya watoto, wanakosa muda wa kuzungumza nao kuhusu masuala ya ukatili hali inayopelekea matukio ya ukatili wa kingono kuongezeka”. Amesema Mkuregenzi Msumi.
Aidha amewataka wanafunzi walioshiriki katika kikao hicho na kupata mafunzo ya namna ya kuzuia ukatili wa kingono kwa kutoa taarifa sehemu husika hasa kwa viongozi wa ngazi mbalimbali kuwa mabalozi wa kusambaza elimu hiyo kwa wanafunzi wenzao huku akiwataka wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao kuhusu masuala ya ukatili.
Hata hivyo, Mkurugenzi Msumi amewaagiza watendaji wa Kata zote za halmashauri yake kuteua wazazi au walezi wa kiume wanne kila Kata kuwa baba wa zamu (Father on Duty) ili kuboresha hatua za kuongea na watoto wa kiume na kuwapatia elimu hasa watoto walio katika kipindi cha balehe kupitia maabara za watoto wa kiume (boys VAC lab) zitakazoanzishwa kwenye shule za msingi.
Kwa upende wake Mkurugenzi wa shirika la CWCD Hindu Mbwego, ameitaka jamii kuwajengea watoto wa kiume uwezo wa kujieleza na kufichua vitendo vya ukatili wa kingono wanavyotendewa na kuepukana na dhana iliyopo ya mtoto wa kiume hatakiwi kuonyesha udhaifu.
“Tukiwajengea watoto wakiume uwezo wa kujielezea yale yanayowasibu tutaweza kuwanusuru na vitendo vya ukatili wa kingono na kuijenga jamii bora Zaidi”. Amesisitiza Mama Hindu.
Aidha, wadau mbalimbali wa kupinga Ukatili wa kingono walioshiriki katika kikao hicho wamelishukuru shirika hilo kwa kuanzisha mradi huo ambao unalenga kuwakomboa watoto wa kiume dhidi ya ukatili wa kingono ambapo kila mmoja kwa nafasi yake ameahidi kutoa ushirikiano katika hatua zote za upelelezi na ufuatiliaji wa matukio ya kingono pale yanapotokea.
Akizungumza katika kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Arumeru Mwamini Kazema, amesema kuwa kuna haja ya kuwajengea watoto uwezo na ujasiri wa kujieleza ili kuwawezesha kupata haki yao ya msingi pale wanapofanyiwa ukatili wa kingono kwani Mhanga wa tukio ndiye shahidi wa kwanza katika kesi hivyo inapotokea mtoto kupata hofu wakati wa kujieleza inapelekea kutoa ushahidi ambao haujajitosheleza.
“Tunaomba vyombo husika kufanyia kazi kwa haraka matukio ya Ukatili wa kingono ili kesi zinazotokana na matukio hayo zisichukue muda mrefu kutoa hukumu ili watoto wapate haki zao na kuepusha mianya ya rushwa au usuluhishi wa kifamilia kutokea” alisisitiza mwalimu wa shule ya Msingi Ilboru Rozina kawahe.
Awali, Shirika hilo la CWCD linatekeleza Mradi wa kuwawezesha watoto wa kiume kuzuia ukatili wa kingono chini ya ufadhili wa shirika la Foundation Civil Society (FCS) katika kata sita za Olturoto, Kiutu, Kiranyi, Oltrumet, Moivo pamoja na Ilboru.
"ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
#kaziinaendelea✍✍✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.