Na. Elinipa Lupembe.
Maelfu ya waombolezaji waliohudhuri kwenye misa takatifu ya kuaga pamoja na mazishi ya aliyekuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha, marehemu Richard Kwitega, wameyaelezea maisha aliyoishi marehemu Kwitega ni maisha ya ushuhuda kwa wengine, hivyo kifo chake kifanyike funzo kwa maisha ya kila mtu.
Akizungumza wakati wa akitoa salamu zake za pole kwa niaba ya Serikali, Naibu Waziri OR -TAMISEMI, mheshimiwa David Silinde, amesema kuwa maisha aliyoyaishi marehemu Kwitega ni maisha ya ushuhuda wa matendo yanayopaswa kufanywa na mtumishi wa Umma katika kuongoza na kutumikia wananchi, pindi anapoaminiwa na serikali na kupata madaraka ya kuwaongoza wengine pamoja na kuwatumikia wananachi.
"Maisha ya Kwitega yawe funzo kwa kila kiongozi na kila mtu, katika kipindi cha uhai wake na utumishi wake, marehemu Richard aliwekeza katika utu, uzalendo na uadilifu, jambo linalotakiwa kufanywa na kila mtumishi wa Umama aliyepewa madaraka na dhamana ya kuongoza na kuwatumikia wananchi, hivyo viongozi tuliopewa dhamana ya kuwatumikia wengine, tuna wajibu wa kutenda mema kwa wale tunaowatumikia" amesisistiza Naibu Waziri Silinde.
Naye Askofu wa Jimbo la Geita, Mhasham Askofu Flavian Kasala, amemuelezea marehemu Kwitega kuwa, aliishi maisha ya kujitoa kwa ajili ya wengine, na kuthibitisha kuwa ana heri yule anayetenda matendo ya imani, matendo ya kujitoa kwa ajili ya wengine na huu ni ushuhuda wa maisha ya marehemu Kwitega kwa kanisa, jamii na serikali aliyokuwa anaitumikia, katika kipindi chote cha maisha yake ya hapa duniani.
Mkuu wa mkao wa Arusha, Mheshimiwa Idd Kimanta, amesema Serikali imepoteza mtu muhimu, hususani katika mkoa wa Arusha, mtu aliyependa kuwatumikia wananchi, kiongozi aliyetekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa bila kubughi wengine, kiongozi aliyejikita zaidi katika ubobevu wake kwenye masuala ya utawala, kifo cha RAS kiwe fundisho katika utumishi wa umma, Kwitega ameondoka akiwa na ushuhuda kwa kila mtumishi mkoani Arusha, tupendane, tuheshimiane, tujaliane na zaidi tubebeane matatizo yetu na kuepuka majungu katika sehemu za kazi.
Katibu Tawala wilaya ya Monduli, Robart Siankeni, amesema kuwa, watamuenzi marehemu Kwitega, kwa kuatekeleza yale aliyowaelekeza ikiwa ni pamoja na kusimamia utawala bora na uwajibikaji katika kuwatumikia wananchi, umuhimu wa kutekeleza mipango ya serikali kwa kusimamia miradi ya maendeleo, kubuni vyanzo vya mapato, kuchochea sekta ya utalii katika mkoa wa Arusha, pamoja na kusimamia amani na utulivu, katika maeneo ya kazi.
Meya wa Jiji la Arusha, Maxmiliani Ilagye amesema kuwa, kifo cha Kwitega ni pigo kwa wananchi wa mkoa wa Arusha, tumepoteza mtu mahiri katika utumishi wa umma, na kuwafariji wafiwa kwa kuwaasa kumtegemea Mungu, "Wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, hawatatikisika, tumuenzi marehemu Kwitega kwa kumtumaini Bwana, hili ni fundisho la kila mmoja kujitathmini na maisha yake ya hapa duniani.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule, amesema kuwa licha ya kuwa marehemu Kwitega alikuwa kiongozi wa kazi kwa watumishi wa mkoa wa Arusha, la zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku, hakuwa boss bali alikuwa kiongozi aliyeshirikiana na watumishi wa mkoa wa Arusha kwa kujipambanua kama rafiki, kaka na baba pia.
Naye mwakilishi wa famili ya marehemu Kwitega na Katibu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ngusa Samike, amesema kuwa, familia inamshukuru sana Mungu kwa zawadi ya maisha ya marehemu Richard Kwitega, kwani alikuwa ni kiongozi wa familia, jamii na kuwa maisha yake yote aliishi kwa kuwatumikia watu.
Marehemu Richard Kwitwega, alifariki kwa ajali ya gari siku ya Jumatano tarehe 03.02.2021, eneo la Mdorii wilaya ya Babati, mkoani Manyara, kwa ajali ya gari, akiwa njiani kuelekea mkoani Dodoma kwa safari ya kikazi.
Marehemu Kwitega amezikwa kijijini kwao, kijiji cha Ngoma kata ya Igalula tarafa ya Nyachenche wilaya ya Sengerema, aidha marehemu Richard Kwitega ameacha Mjane na watoto wanne.
BWANA ALITOA BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE!
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.