Mkuu wa wilaya ya Arumeru mheshimiwa Jerry Muro amewataka maafisa ugani wa wilaya ya Arumeru kushirikiana kwa karibu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania 'Tanzania Agricultural Reseach Institute - TARI' kuwezesha wakulima kulima kilimo chenye tija chenye kuzalisha mazao bora.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa rai hiyo, alipokutana na Mafisa Ugani wa kata 53, kata zinazojumuisha halmashauri mbili za Arusha na Meru wilayani Arumeru, wakati wa kikao kazi, ambacho mheshimiwa Muro amekiita kikao cha mkakati wa kilimo katika wilaya yake, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano shule ya msingi Green Acress.
Mheshimiwa Muro ameongeza kuwa, licha ya kuwa TARI inahudumia Tanzania nzima lakini kwa kuwa makao makuu yapo wilayani Arumeru, kuna ulazima wa wilaya ya Arumeru, kuwa eneo la mfano, ambalo wakulima wataachana na kilimo cha mazoe, na kujikita kwenye kilimo cha kimkakati, kitakachomtoa mkulima kwenye lindi la umasikini kwa kumuwezesha mkulima wa Arumeru kulima kilimo chenye kutumia mbegu bora na kuweza kupata mazao bora.
"TARI wanafanya tafiti za mbegu za mazao ya hot culture ' kituo kipo Tengeru kwa nini wakulima wetu wasinufaike na kituo hicho? Kuna sababu gani wakulima wangu waendelee kupata hasara kupitia shughuli za kilimo wanazozifanya? Amehoji mheshimiwa Muro
Aidha amesema kuwa lengo lake, katika kuelekea uchumi wa viwanda ni kuhakikisha wakulima wa Arumeru, wanalima kilimo cha kimkakati chenye kutumia mbegu bora na kupata mazao bora yenye uwezo wa kuchakatwa na kuongezewa thamani kupitia viwanda vyetu vya ndani na kuuzwa kama bidhaa ghafi na si kuuza mazao kama ilivyozoeleka.
Na kuagiza Maafisa hao kuandaa taarifa itakayoonesha idadi ya wakulima waliopata ujuzi ikiwa na namba zao za simu ili aweze kuwasiliana nao kuthibitisha endapo ni kweli wakulima hao kupata ujuzi huo wa kilimo.
Naye Meneja wa kituo cha utafiti wa kilimo Tanzania -TARI amesema kuwa, yuko tayari kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru, kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanalima kimkakati na kuwezesha nchi yetu kuelekea uchumi wa viwanda huku kilimo hicho kikimnufaisha mkulima kwa kumuongezea kipato.
Dkt. Sebastian amefafanua kuwa, taasisi hiyo inatoa huduma kwa watanzania wote ikiwemo wakulima binafsi, taasisi binafsi na za serikali pamoja na makampuni hivyo ni dhahiri kupita watalamu wa taasisi hiyo, wakulima wananafasi kubwa ya kubadili aina ya kilimo na kulima kilimo chenye tija.
Ametaja mazao yanayofanyiwa tafiti ni pamoja na mazao ya mboga, matunda na mazao ya mizizi na kuongeza kuwa, kupita tafiti hizo wamefanikiwa kupata mbegu bora na zinazozalishwa mazao bora.
Hata hivyo Maafisa Ugani hao, wamempongeza mkuu huyo wa Wilaya, kwa kukaa nao kirafiki na kuwatia moyo juu ya utekelezaji wa majukumj yao,na zaidi kupanga mikakati na mipango ya pamoja, yenye lengo la kuboresha hali ya kilimo kwa manufaa ya wananchi wa Arumeru na taifa kwa ujumla.
Afisa Kilimo kata ya Oloirieni, Justine Ishemwabura, amesema kuwa kikao kazi hicho, kimewapa mwelekeo wa nini cha kufanya ili kuwafikisha wakulima kwenye kilimo chenye tija
" Nimefurahishwa na kikao hiki, kimsingi kimetupa hamasa ya kufanyakazi, tunaahidi tunakwenda kufanya kazi, kupitia mambo mbalimbali tuliyokumbushana na malengo tuliyojiwekea malengo, ambayo ni rahisi kuyapima baada ya kipindi flani" amesema Afusa Kilimo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.