Na.Elinipa Lupembe
Maafisa ugani wametakiwa kuzingatia weledi katika ufanyaji kazi wao kwa kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma wakati wote katika utekelezaji wa jukumu kubwa la kuwahudumia wakulima katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa kwenye kikao kazi kilicho jumuisha maafisa kilimo wa kata na vijiji katika halmashauri ya Arusha ikiwa ni sehemu ya kutathimini na kukumbushana juu ya utekelezaji wa majukumu ya kuwahudumia wananchi hususani wakulima.
Mkuu wa Idara ya Utumishi na Rasilimali Watu, halmashauri ya Arusha, Elizabeth Ngobei, amewakumbusha maafisa hao kuwajibika kwenye maeneo yao ya kazi kwa kuwahi kazini, kutekeleza majukumu ya siku, kuzingatia muda wa masaa ya kazi pamoja na kuzingatia sheria zote za kazi.
Ngobei amesema kuwa, Serikali imewapa dhamana ya kuwahudumia wananchi ambao zaidi ya asilimia 70 ni wakulima na wafugaji, hivyo wanalo jukumu kubwa la kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa hili kupitia fani hiyo ya kilimo.
Aidha amewataka maafisa hao kutambua kuwa, Serikali inawathamini watumishi wote kwa kuzingatia haki za mtumishi mmoja mmoja ikiwemo kulipa mishahara na stahiki nyingine kama kuwapa nafasi ya kujiendeleza kitaaluma, ili kujiongezea maarifa pamoja na kuhakikisha wanapata likizo ya mwaka ambayo inagharamiwa na Serikali kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.
“Niwatake watumishi kufanya kazi kwa weledi pamoja na kutumia fursa ya kwenda masomoni na kujiendeleza kielimu, jambo ambalo linawaweka kwenye nafasi nzuri na ya juu zaidi katika masuala mazima ya maslahi yenu ya utumishi wa umma”, amesisitiza.
Awali, Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo Omary Sembe, amesema kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kukumbushana majukumu ya kazi pamoja na kupeana maelekezo ya serikali ili kuwa na uelewa wa pamoja lengo likiwa ni kuyafikia malengo yaliyowekwa.
“Serikali imekusudia kuwawezesha Maafisa Ugani, kwa kuwapa vitendea kazi kama pikipiki, vipima afya vya udongo, mfumo wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima, hivyo maafisa kilimo mnalo jukumu la kuhakikisha mnawawezesha wakulima kufikia malengo ya serikali kwa kuongeza pato la mkulima”, Amesema.
“Serikali imekusudia kuwawezesha Maafisa Ugani, kwa kuwapa vitendea kazi kama pikipiki, vipima afya vya udongo, mfumo wa ruzuku ya mbolea kwa wakulima, hivyo maafisa kilimo mnalo jukumu la kuhakikisha mnawawezesha wakulima kufikia malengo ya serikali kwa kuongeza pato la mkulima”, Amesema.
.Hata hivyo Maafisa Ugani hao wamekiri kuwa kikao kazi hicho ni muhimu kwao, kwa licha ya kuwakumbusha utekelezaji wa majukumu yao, zaidi kinatoa dira ya namna bora ya kuyafikia malengo ya Serikali yanayoenda na wakati, mabadiliko ya tabia nchi sambamba na mabadiliko ya Sayansi na teknolojia yakiwa na lengo la kuhakikisha wakulima wanapata huduma bora na stahiki kutoka kwao watalamu wa kilimo.
Halmashauri ya Arusha imetenga shilingi milioni 35 kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu ya skimu za umwagiliaji katika kata ya Bwawani, vilevile Serikali imewarahisishia maafisa kilimo usafiri ili kuwatembelea wakulima vijijini na kufanya kilimo endelevu kinachowawezesha wakulima kuwa na mashamba darasa kwa kupewa mbegu, mbolea na viwatilifu ili kupata mazao bora kwa mwaka mzima.
ARUSHA DC NI YETU, TUSHIRIKIANE KUIJENGA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.