Na. Elinipa Lupembe.
Mdau wa maendeleo na mtalii kutoka nchini Marekani, bwana Claude Piere, amekabidhi msaada wa vifaa vya kujifunzia na kujifunzia pamoja na kupaka rangi vyumba 10 vya madarasa, shule ya msingi Olimringaringa, halmashauri ya Arusha.
Mdau huyo wa maendeleo, ambaye ni rafiki wa shule hiyo, ameweka wazi kuwa, amefikia uamuzi huo baada ya kuona uhitaji wa watoto wa shule hiyo, kusoma katika mazingira yanayovuti na pamoja na kuwa na vitabu vya kutosha, vitakavyoweza kuwapa maarifa zaidi.
"Elimu ndio zawadi kubwa ya pekee kwa watoto wa shule ya msingi Olimringaringa, itakayowawezesha kupata maarifa, wote tumepata elimu, napenda kutoa zawadi hii iweze kuwasaidia, wanafunzi kuwa na maisha ya furaha wawapo shuleni" amesisitiza Claude.
Mwalimu mkuu shule ya msingi Olimringaringa, Revokatus Gamba, licha ya kumshukuru mdau huyo kwa kutoa msaada huo wa kupaka rangi vyumba vya madarasa na baadaye kutoa msaada huo wa vitabu, amefafanua kuwa, msaada huo utaongeza hamasa kwa wanafunzi kujisomea na kupata maarifa na hatimaye kuwawezesha kufaulu vizuri katika mitihani yao na kupandisha kiwango cha taaluma shuleni hapo.
"Tunamshukuru bwana Pierre kwa kupaka rangi vyumba kumi vya madarasa, madarasa ambayo yalikuwa yameanza kuchakaa kutokana na kujengwa muda mrefu, mazingira ya shule sasa yanavutia wanafunzi kusoma na walimu kufundishia, yanaongeza hamasa ya kujifunza" amesema mwalimu huyo.
Naye mratibu wa mradi huo, Vicky Laizer amesema kuwa, mtalii huyo, ametoa vifaa hivyo kupitia mradi unaojulikana kama 'Olimringaringa Primary school Donation Project', wenye lengo la kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi wa kuanzia darasa la awali mpaka shule ya msingi.
Aidha amevitaja vifaa alivyokabidhi shuleni hapo ni pamoja na kalamu, rula, vichongeo, vitabu vitabu vya hadithi vya lugha ya kingereza, vinavyowezesha wanafunzi kujiongezea maarifa ya ziada katika masomo na pamoja na kujifunza lugha ya kiingereza, pamoja na kupaka rangi vyumba 10 vya madarasa.
Hata hivyo wanafunzi wa shule hiyo ya msingi, wamemshukuru mdau huyo, kwa kuona umuhimu wa kuboresha mazingira ya shule yao pamoja na kuwapa vifaa vya kujifunzia na kufundishia ikiwemo vitabu vya kiada na ziada.
Bahati Olais mwanafunzi wa darasa la sita, amemshukuru mdau huyo na kuthibitisha kuwa, kwa sasa vyumba vya madarasa vinavutia na vinawapa hamasa ya kusoma, na vitabu walivgopewa vitawawezesha kusoma na kuahidi kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu vizuri.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.