Na. Elinipa Lupembe
Baraza la Madiwani halmashauri ya Arusha, limepitisha Mpango wa Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka ujao wa fedha 2023/2024, kwenye mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani ulliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano halmashauri ya Arusha.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Mwenyekiti wa Mkutano huo,na Diwani wa kata ya Olturoto Mhe. Baraka Simon, amethibitisha baraza hilo kupitisha Mpango wa bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka ujao wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 60.2, kwa kuwataka watalamu, kuboresha vyanzo vya mapato vilivyopo na kuimarisha mkakati wa ukusanyaji mapato huku wakiendelea kubuni vyanzo endelevu vya mapato vitakavyowezesha utekelezaji wa bajeti iliyopitishwa kiuhalisia.
"Ninawapongeza watalamu wa ngazi zote, ofisi ya mkuu wa wilaya Arumeru, waheshimiwa madiwani na wadau wote wa maendeleo kwa ushirikiano wao unaowewezesha kusukuma gurudumu la maendeleo la halmashauri yetu, licha ya changamoto nyingi lakini bado utekelezaji wa malengo ya halmashauri unafanyika kwa kasi" amesema Mwenyekiti huyo.
Aidha Mheshimiwa Mwenyekiti huyo, ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia kwa kuendelea kuleta fedha nje ya bajeti na kutekeleza miradi mikubwa katika halmashauri hiyo, ikiwemo miradi ya maji, barabara, umeme, elimu na afya, miradi ambayo kupitia mapato ya halmashauri peke yake isingeweza kutekelezeka.
Awali akiwasilisha Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Mapato na Matumizi ya kwa mwaka ujao wa fedha 2023/2024 mbele ya wajumbe wa Baraza la Waheshimiwa Madiwani, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu halmashauri ya Arusha, Anna Urio, amesema kuwa, halmashauri inategemea kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 60.2 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.
Afisa Mipango huyo ameainisha mchanganuo wa bajeti hiyo ya bilioni 60.2, itahusisha mapato ya ndani kiasi cha shilingi bilioni 5.6, Ruzuku ya mishahara (PE) shilingi bilioni 42.7, Ruzuku ya matumizi mengine (OC) shilingi bilioni 1.7 huku Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo ikiwa ni shilingi bilioni 12.
Hata hivyo Afisa Mipango huyo, amesema kuwa mpango huo wa bajeti umeandaliwa kwa mujibu wa sheria ya bajeti sura 439 na kanuni zake za mwaka 2015 pamoja na Kanuni zake, maelekezo na mwongozo wa kitaifa maandalizi ya Bajeti, unaoelekeza kupokea mapendekezo na vipaumbele kisekta kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, Idara na Vitengo vya halmashauri.
Ameongeza kuwa, halmashauri imefanya Mpango wa Bajeti hiyo, kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya mwkaa 2022/2023 kwa mujibu wa Sheria na Maelekezo na Mwongozo wa kitaifa lakini pia imezingatia Mpango shirikishi wa Jamii, Mpango mkakati wa halmashauri wa mwaka 2021/2024 mpaka 2025/2026 na vipaumbele vya halmashauri kisekta kwa kuzingatia maeneo yatakavyoleta msukumo katika Uchumi na huduma Bora za Jamii na Utawala Bora.
Aidha Afisa Mipango Ana ameendelea kufafanua kuwa, katika mpango huo wa Bajeti umejikita pia katika kutekeleza shughuli zinazolenga kutekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA III) na na kuzingatia 'Tanzania Development Vission 2025' zinazosisitizwa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, Mpango wa Taifa wa Miaka mitano, Malengo ya maendeleo endelevu, (SDG's) ya 2030.
Awali katika mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha unaoendelea wa 2022/2023 halmashauri ya Arusha iliidhinishiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kukusanya na kutumia jumla ya shilingi Bioni 59.5, ikiwa mapato ya ndani shilingi Bilioni 4.8, Ruzuku ya miradi ya maendeleo bilioni 10.7, Ruzuku ya mishahara shilingi bilioni 42.8, Ruzuku ya matumizi ya kawaida shilingi Bilioni 1.1.
"ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
KaziInaendelea✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.