Madiwani kutoka Kaunti ya Bungoma nchini Kenya, wamefurahishwa na kuridhishwa na hali ya usafi wa mazingira waliojionea wenyewe, kwenye maeneo waliyopita, wakiwa kwenye ziara yao ya mafunzo kwenye Halmashauri za Arusha na Jiji la Arusha na mkoa wa Arusha kwa ujumla.
Madiwani hao wamesema hayo, wakati wa kikao kifupi cha kubadilishana uzoefu na Madiwani wa halmashauri ya Arusha, kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi mdogo wa Mwenyekiti, halmashauri hapo.
Katika kikao hicho, madiwani hao wa Bungoma, kutokana na hali ya usafi wa mazingira walijionea katika maeneo waliyopita, ikawalazimu kuhoji, utaratibu unaotumika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi licha ya msongamano wa watu katika miji hiyo.
Akitoa ufafanuzi wa jitihada hizo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha, Mhe. Noah Lembris , amewaelezea madiwani hao kuwa, halmashauri ina sheria ndogo za usafi wa mazingira zinazoruhusu kumtoza faini mwananchi atakayetupa takataka mahali pasipo husika, na kuongeza kuwa halmashauri imeweka mawakala wanaokusanya taka kwenye maeneo ya miji ambayo mwananchi huchangia kiasi cha fedha za uzoaji takataka.
Hata hivyo Mwenyekiti Noah, ameongeza kuwa kuna utaratibu wa kufanya usafi wa jumla kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi huku watalamu na viongozi wa maeneo husika, wakisimamia zoezi hilo.
Hata hivyo, licha ya madiwani hao kupendezwa na hali ya usafi lakini pia walitaja kubadilishana uzoefu, juu ya utaratibu mzima wa uendeshaji wa halmashauri, ikiwemo utoaji wa huduma kwa wananchi, utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kusanyaji wa mapato.
Mwenyekiti Noah alipata fursa pia ya kuelezea kuwa uendeshaji wa halmashauri unaanzia ngazi ya chini kabisa ya kitongoji, na kufuatia kijiji, kata, tarafa mpaka ngazi ya halnashauri.
Mgawanyo huo wa madaraka kuanzia ngazi ya chini, unawezesha halmashauri kujiendesha na kuweza kusimamia miradi ya maendeleo pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi huku maamuzi ya wananchi yakifanyika kwenye mkutano mkuu wa kijiji ambao hufanyika mara nne kwa mwaka.
Naye Spika wa Kaunti ya Bungoma, Mhe. Emmanuel Situma, amepongeza utekelezaji wa majukumu ya halmashauri ya Arusha na serikali ya Tanzania katika kuwahudumia wananchi kupitia muundo wa halmashauri pamoja na ushiriki wa wananchi wa ngazi ya chini kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika huyo, amethibitisha ulinganifu uliopo wa Tanzania na Kenya katika uendeshaji wa halmashauri licha ya utofauti uliopo wa upatikanaji wa viongozi akiwemo spika ambaye hatokani madiwani, viongozi wa wakuchaguliwa na wananchi na wale wa kuteuliwa.
Jumla ya Madiwani 13 wa Kaunti ya Bungoma wamefanya ziara ya mafunzo kwenye halmashauri za Jiji la Arusha na halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kuendesha halmashauri.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.