Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe.Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, ameongoza zoezi la uteketezaji wa jumla ya Magunia 237 ya Dawa za kulevya aina ya bangi, kutoka maeneo tofauti tofauti ndani ya Wilaya ya Arumeru. Zoezi hilo limefanyika katika Dampo la Kikatiti halmashauri ya Meru. Wakati wa uchomaji wa bangi hilo, Kaganda aliambatana na kamati ya Usalama Wilaya ya Arumeru pamoja na Maafisa kutoka ofisi ya Kanda inayoshughulikia udhibiti wa dawa za kulevya Mkoani Arusha.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mhe.Kaganda amesema mwezi Septemba na Oktoba mwa huu, waliongoza oparesheni na kufanikiwa kukamata Magunia ya bangi 316 ambapo magunia 91 yalishateketezwa na yaliyobaki 237 yameteketezwa leo pamoja na kilo 310 za mbegu za bangi.
Mhe.Kaganda amesema, mpaka sasa uzalizaji wa zao la bangi kwa maeneo ya Kisimiri na Losinon juu umepungua kutokana na juhudi za Serikali kutoa elimu ya madhara ya zao hilo.
"Kama Serikali tutahakikisha tunaendelea kupambana na wale wote wanaojihusisha na ulimaji wa zao hili, ni muhimu kutambua kuwa Arumeru siyo sehemu salama kulima, kuuza au kutumia bangi. Natoa wito kwa wakulima wetu, kujihusisha na kilimo cha mazao mengine na tayari Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inao mkakati juu ya ulimaji wa zao mbadala la Pareto na mazao mengine yatakayofaa kutokana na hali ya hewa ya Arumeru"
Sambamba na hilo, Mhe.Kaganda amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama Wilayani Arumeru pamoja na wananchi kwa ushirikiano katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ikiwemo kilimo cha bangi. Pia ameweka wazi kuwa zoezi hilo ni ajenda ya kudumu ili kuhakikisha jamii inabakia salama na kwamba Arumeru bila Bangi inawezekana.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.