Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kukamilisha mchakato wa kusanifu na kujenga Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini na kuhakikisha Taasisi zote za umma zinajumuishwa katika mfumo huo.
Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Tano cha Mamlaka ya Serikali Mtandao kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC). Amesema Jambo hilo ni muhimu ili kurahisisha utendaji kazi katika taasisi na kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Taasisi za Umma kuhakikisha kuwa mifumo yao inasomana na kubadilishana taarifa.
Aidha Makamu wa Rais amesema Taasisi zote za umma zinapaswa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao katika hatua zote za ujenzi au ununuzi, usimamizi na uendeshaji wa Miradi ya TEHAMA pamoja na kuwataka kuwaelekeza Wakuu wote wa taasisi za umma kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na Mamlaka husika katika utekelezaji wa shughuli za Serikali Mtandao.
Hali kadhalika, Makamu wa Rais ameagiza mikoa ambayo bado haijaanza kutumia utaratibu wa Ofisi ya Kielektroniki (e-office) kuhakikisha wanaaanza kutumia mfumo huo ifikapo tarehe 30 mwezi juni. Aidha ameagiza kituo cha utafiti kiweze kuimarishwa pamoja na kuongezewa eneo la ufanyaji kazi.
Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA na kada nyingine, kwa kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji katika Vyuo Vikuu na Taasisi za elimu ya juu ili viendelee kuzalisha wataalam wa kutosha.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.