Na. Elinipa Lupembe.
Msahiki Meya wa Jiji la Arusha Mheshimiwa Maximilian Iranghe, amekuwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania - ALAT mkoa wa Arusha, mara baada ya kuibuka kidedea kwa kumshinda mpinzani wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Monduli, kwenye uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa kikao hicho na Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, mheshimiwa Ojung'u Salekwa, amesema kuwa katika uchaguzi huo, mheshimiwa Maximilian Iranghe amepata kura 15 kati ya kura 28 zilizopigwa na kumshinda mpinzani wake Mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli, mheshimiwa Isack Capricorn aliyepata kura 13.
"Kwa Mamlaka niliyopewa, kwa mujibu wa sheria na kanuni za serikali za mitaa, na kutokana na matokeo hayo kura zilizopigwa, ninamtangaza Meya wa Jiji la Arusha, mheshimiwa Maximilian Iranghe kuwa Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Arusha, na kuiongoza jumuia hiyo kwa kipindi cha miaka mitano" ametangaza Mheshimiwa Salekwa.
Akizungumza baada ya kutangazwa, Mwenyekiti mpya wa ALAT mkoa wa Arusha, mheshimiwa Maximilian Iranghe, licha ya kuwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumchagua, amewataka kufanyakazi kwa kushirikiana kama timu, imani ambayo anaamini itawezesha kufikia lengo moja la kuwatumikia wananchi wa mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.
"Ninaamini katika kufanyakazi kwa kushirikiana pamoja, nanukuu usemi usemao 'ukitaka kufika haraka nenda peke yako, lakini ukitaka kufika mbali nenda na wenzako', kama viongozi na wawakilishi wa wananchi lengo letu ni kuitoa ALAT hapa ilipo na kuipeleka mbali zaidi kufuatia malengo na mipango ya tuliyojiwekea kwa maslahi ya wananchi na taifa letu la Tanzania "amesisitiza Mwenyekiti huyo mpya wa ALAT mkoa wa Arusha.
Hata hivyo katika uchaguzi huo, nafasi ya Makamu mwenyekiti, imechukuliwa na mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, mheshimiwa Ojung'u Salekwa, huku nafasi ya Katibu ikichukuliwa na mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya wilaya ya Karatu, wakati nafasi ya mbunge mwakilishi ALAT mkoa, ikichukuliwa na Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, mheshimiwa Noah Lembris.
Aidha katika mkutano huo, kikanuni wajumbe waliwachagua wajumbe watano wa Kamati tendaji, ambapo mhe. Glory Kaaya Diwani mwakilishi, halmashauri ya Meru, Mhe.Isaya Doita, Diwani mwakilishi halmashauri ya Jiji la Arusha, Mhe. John Mahuu, Mwenyekiti wa halmashauri ya Karatu, Mhe. Miryam Kissamike Diwani mwakilishi Jiji la Arusha, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Monduli, Steven Ulaya.
Jumuia ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania katika ngazi ya mkoa, inayoundwa na mameya wa majiji, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri, wabunge wa majimbo yote pamoja na madiwani wawakilishi wawili kutoka katika halmashauri saba za mkoa wa Arusha.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.