Na OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwekeza kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kupitia Michezo, Utamaduni na Sanaa ili kuwarithisha na kuwajenga kuwa mabalozi wazuri wa kudumisha jumuiya hiyo.
Amesema hayo leo Septemba 23, 2022 wakati akifunga Mashindano ya 20 ya michezo ya shule za msingi na za Sekondari kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSSA GAMES) katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Amehimiza Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka mpango mahsusi na bunifu wa kuelimisha wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kupitia Michezo, Utamaduni na Sanaa juu ya umuhimu wa Jumhiya na kuendelea kuenzi tamaduni zilizopo.
Bashungwa amesema Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatambua umuhimu wa michezo kwa watoto na vijana na zitaendelea kugharamia michezo shuleni katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na mashindano ya shule za msingi na Sekondari za Afrika Mashariki (FEASSSA)
Bashungwa ametoa wito kwa viongozi wa mashirikisho ya kila nchi mwanachama wa FEASSSA, kufanya tathmini ya maendeleo ya mashindano hayo, ikiwa ni pamoja na kubaini changamoto walizokutana nazo na ikibidi kutoa mapendekezo ya pamoja kuhusu namna ya kuunganisha nguvu ili kuboresha mashindano hayo.
Amesema nchi wanachama zinaendelea kunufaika na ushirikiano uliopo katika nyanja za elimu, sayansi, jamii, uchumi, utamaduni na michezo na amehimiza umoja na mshikamano ili kukuza na kuendeleza michezo kwa pamoja.
Aidha, Bashungwa amesema sasa imefika wakati wa FEASSSA kupanua wigo kwa kuongeza mafunzo ya ufundishaji michezo, uamuzi wa michezo, tiba ya wanamichezo, utawala wa michezo, na kuongeza eneo la utamaduni katika mashindano ili kuenzi na kulinda utamaduni wetu kupitia ngoma za asili, kwaya na ubunifu.
Vile Vile, Bashungwa amewapongeza walimu na waandaaji wa mashindano kutoka katika nchi za Uganda, Kenya, Rwanda na Tanzania kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuwaandaa wanamichezo katika fani mbalimbali zilizokuwa zinashindaniwa katika mashindano hayo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.