Na. Elinipa Lupembe.
Serikali kipitia programu ya lipa kutokana na matokeo (P4R), imetoa kiasi cha shilingi milioni 200, kukamilisha na kupanua ujenzi wa miundombinu ya zahanati ya kijiji cha Musa, kata ya Musa, halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru, jengo ambalo lilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji hicho.
Lengo la mradi huo likiwa ni utekelezaji mkakati wa serikali ya awamu ya tano wa kuhakikisha, huduma muhimu za afya zinawafikia wananchi katika maeneo yao, kwa kila kijiji kuwa na zahanati, kata kuwa na kituo cha afya, wilaya kuwa na hospitali ya wilaya kadhalika kila mkoa kuwa na haspitali ya Rufaa, jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mganga mkuu halmashauri ya Arusha Dkt. Peter Mboye, ameeleza kuwa mradi huo ni muhimu kwa wananchi wa kijiji cha Musa na vitongoji vyake, licha ya uchakavu wa jengo la zahanati iliyokuwepo kuendelea kutoa huduma, lakini pia jengo hilo lilikuwa dogo, lisilokidhi mahitaji, kulinganisha na idadi ya wateja wanaohudumiwa katika zahanati hiyo kwa siku.
Dkt. Mboye amefafanua kuwa, kiasi hicho cha fedha kimetumika kumalizia jengo la zahanati ambalo lilianzwa kujengwa na wananchi, jengo ambalo limebeba sehemu ya wagonjwa nje 'OPD', maabara, kliniki ya mama na mtoto, nyumba ya daktari pamoja na vyoo vya nje, ujenzi ambao unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu wa 2020.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Musa, Ernest Lesikari, pamoja na kuishukuru serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, amethibitisha umuhimu wa mradi huo kwa wananchi, si wa kijiji cha Musa pekee yao, bali na wananchi wa vijiji jirani vya kata nzima ya Musa.
"Jengo la zahanati lililopo, lilijengwa miaka mingi iliyopita, kukiwa na idadi ndogo ya watu, lakini tayari limechakaa, na halitoshi kuhudumia wagonjwa wengi kulingana na idadi kubwa ya wagonjwa waofika zahanati hapo kupata huduma kila siku "amesema Mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa, tangu serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani, hali ya upatikanaji wa huduma za afya katika zahanati hiyo zimeimarika kwa kiasi kikubwa, ikiwemo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, huduma za kujifungua kwa wajawazito, kliniki ya mama na mtoto pamoja na huduma zote muhimu tofauti na miaka ya nyuma.
Namnyaki Matayo, mkazi wa kijiji cha Musa, amesema kuwa, ujenzi wa zahanati hiyo, umeleta matumaini makubwa kwa wanawake wa kijiji hicho, kwa kuwa wao ndio walezi wa familia, ambao mara nyingi, huteseka wakati wa kujifungua na kuhudumia wagonjwa ndani ya familia zao.
"Kina mama ndio hupata mateso hasa wakati wa kujifungua, na sisi ndio tunakimbizana na wagonjwa wa familia, mara hospitali ya Monduli, Olturumeti lakini sasa tuna nerma tunapata huduma bora hapa karibu, kina mama tutapumzika sasa" amesema Namnyaki
Awali ujenzi wa Zahanati hiyo, umeanza mwezi wa Machi na unategemea kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Juni na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa kata ya Musa na Vitongoji vyake.
PICHA ZA MAJENGO YA ZAHANATI HIYO
Msingi wa nyumba ya Daktari.
Jengo la zahanati ya zamani kijiji cha Musa
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.