Halmashauri ya Arusha imeanza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu, baada ya serikali kuongeza fedha nyingine kiasi cha sh milioni 480, fedha za mradi wa lipa kutokana na matokeo (Payment for Result 'P4R').
Fedha hizo zimekuja mara baada ya halmashauri hiyo, kukamilisha kwa umakini na kwa wakati, mradi wa awali wa P4R wenye thamani ya shilingi milioni 500.
Kiasi hicho cha fedha cha shilingi milioni 480, kimetolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati miundo mbinu ya shule kufuatia adhma ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na shule zenye miundombinu na mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, wakati akikagua maendeleo ya miradi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera amekiri kupokea kiasi cha shilingi milioni 480 na kueleza kuwa fedha hizo zinatumika kwa shule za msingi na sekondari kwa mgawanyo unaokaribiana.
Dkt. Mahera amefafanua mgawanyo wa fedha hizo kuwa, kiasi cha shilingi milioni 227 zitatumika kwa shule za msingi, ambapo milioni 96 zinatumika kujenga vyumba vinne vya madarasa, kwa gharama ya shilingi milioni 24 kwa kila darasa pamoja na kununua madawati katika madarasa hayo.
Aidha shilingi milioni 96 nyingine zitatumika kusawazisha ikama ya walimu na milioni 35 zitatumika katika ukusanyaji wa takwimu muhimu za shule zote za msingi, takwimu zitakazosaidia kupata picha halisi ya hali ya shule, wanafunzi na uendeshaji wa shule wenye lengo la kuendelea kufanya maboresho katika suala zima la elimu shuleni.
Ameendelea kueleza kuwa kiasi kingine cha shilingi milioni 253 kinatumika kukarabati na kumalizia miundombinu ya maabara za sayansi kwenye jumla ya shule 7 za sekondari pamoja na kujenga vyumba 5 vya madarasa kwenye shule nne za sekondari.
Aidha Dkt. Mahera amethibitisha kuwa, miradi yote imeanza kutekelezwa kwa kasi kwenye shule zote zilizoainishwa na kuongeza kuwa, kukamilika kwa miundombinu hiyo ya shule, kutaongeza ufanisi na ari ya wanafunzi kujifunza na walimu kufundisha, jambo ambalo anaamini litapandisha kiwango cha taaluma katika shule hizo.
Naye Afisa Elimu Sekondari, halmashauri ya Arusha, mwalimu Sofia Msofe amesema kuwa, kukamilika kwa maabara katika shule za sekondari kutaleta tija na hamasa kwa wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi kutokana kujifunza kwa nadharia na vitendo pia.
"Mimi ni mwalimu wa Biolojia, masomo ya Sayansi bila kufanya kwa vitendo ni kubahatisha, lakini once mwanafunzi akijifunza kwa nadharia akafanya kwa vitendo ni rahisi kuelewa na kukumbuka, na zaidi kulipenda somo" amesema Afisa Elimu huyo.
Nakuongeza kuwa awali masomo ya Sayansi yalikuwa yanafundishwa kwa kufanya 'alternative to practical' jambo ambalo wanafunzi walikuwa wanalazimika kukariri zaidi bila kuelewa, lakini uwepo wa maabara, wanafunzi sasa watafanya kwa vitendo na kwa uhalisia zaidi jambo ambalo licha ya kuongeza uwelewa wanafunzi pia hufurahia somo.
Awali fedha za P4R kiasi cha shilingi milioni 500, zilitumika kujenga vyumba 8 vya madarasa ya kidato cha 5&6, ukarabati wa maabara za sayansi, mabweni ya wasichana na vyoo kwenye shule za sekondari Mlangarini na Mwandeti, mradi ambao ulikamilika kwa wakati na tayari wanafunzi wanafaidika na matunda ya mradi huo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.