Mikakati ya halmashauri ya Wilaya ya Arusha, chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dkt. Wilson Mahera, ya kupandisha kiwango cha taaluma na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi, imeanza kuzaa matunda mara baada ya wanafunzi wa darasa la saba walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2018, kufaulu kwa asilimia 89%.
Matunda hayo mema, yamejidhihirisha wazi baada ya ongeeko kubwa la ufaulu la asilimia 18% na kupanda kwa nafasi 76 na kufikia kiwango cha ufaulu cha asilimia 89%, katika matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba, mwaka 2018, kama matokeo hayo yalivyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani 'NECTA'.
Akizungumza ofisini kwake, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, amepata fursa, ya kuelezea sababu zilizopelekea kupanda kwa kiwango cha taaluma shuleni, amesema kuwa ni pamoja na juhudi kubwa za utekelezaji wa mpango mkakati waliojiweke ndanibya halmashauri yao kupitia Idara ya Elimu, juhudi ambazo zimewezesha ongezeko kubwa la ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba kwa mwaka huu.
Mkurugenzi huyo, ametaja kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa darasa mwaka 2018 kuwa, kimepanda kutoka asilimia 71% ya mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 89%, na kuifanya halmashauri hiyo, kushika nafasi ya 21 kitaifa kati ya halmashauri 185 za Tanzania kutoka nafasi ya 97 ya mwaka 2017, huku ikishika nafasi ya 2 kati ya halmashauri 7 za mkoa wa Arusha.
Aidha Dkt. Mahera amethibitisha kuwa, ufaulu huo wa wanafunzi unaendelea kuimarika na kupanda kila mwaka ukilinganishwa na miaka mitatu ya nyuma, kutokana na mipango na mikakati mizuri iliyowekezwa, kwenye sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa walimu, wanafunzi pamoja na wazazi.
Dkt. Mahera, ameitaja siri kubwa iliyopelekea halmashauri hiyo kupata mafanikio hayo, ni kujituma kila mmoja kwa nafasi yake, pamoja na utekelezaji thabiti wa mipango mikakati, inayoenda sambamba na kufanya kazi kwa bidii na kwa kushirikiana kama timu kwa sekta zote zinazohusika na masuala ya elimu
"Nilipofika hapa walimu walikuwa wamekata tamaaa, lakini nilijitahidi kukaa na kuzungumza nao, kutatua changamoto ndogondogo zilizokuwa zikiwakabili, na kubwa zaidi ilikuwa ni kuwatia moyo, kwa kuwa niliamini kazi ya kubwa ya kupandisha ufaulu, inafanywa na walimu hivyo walimu wakiwa demoralized, ufaulu haupo, lakini walimu wakijituma kwa moyo lazima wanafunzi watafanya vizuri katika mitihani yao, na ndicho kilichotoke". alieleza Dkt.Mahera.
Ameongeza kuwa sababu nyingine iliyopelekea halmashauri ya Arusha kupata mafanikio hayo makubwa, ni ushirikiano mzuri, uliopo baina ya uongozi wa halmashauri kuanzia ngazi ya wilaya, kata, kijiji mpaka ngazi ya uongozi wa shule pamoja na walimu wenyewe.
" Tunafanya kazi kama timu na kuwekeana malengo, kuanzia ngazi ya halmashauri, Maafisa Elimu kata kuhakikisha wanawafuatlia walimu na kusimamia ufundishaji shuleni, na walimu kuhakikisha wanatimiza wajibu wao, wa kuwafundisha wanafunzi kulingana na mitaala inavyoelekeza, lakini mwishoni tunapima malengo tuliyojiwekea, kupitia kitengo cha Ukaguzi na Uthibiti ubora wa Elimu"
Mkurugenzi huyo, amewapongeza walimu, Maafisa Elimu kata, Idara ya Elimu, Kitengo cha Ukaguzi na Uthibiti Ubora, wanafunzi pamoja na watumishi wote wa halmashauri ya Arusha, kwa kazi nzuri wakiyoifanya ya kuwezesha ufaulu huo, na kuwataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuweka uzalendo mbele.
Dkt. Mahera amefafanua kuwa, mkakati wa kupandisha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi haupo kwenye elimu ya msingi pekee bali halmashauri pia imeweka mkakati wa kufuta alama sifuri kwa wanafunzi wa kidato cha nne, kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anapata walau 'D' nne katika mitihanj yake, na kuongeza kuwa mkakati huo ulileta matokeo mazuri kwa mwaka 2017, halmashauri ilishika nafasi ya 31 kitaifa kutoka nafasi ya 79 mwaka 2016 na kuwa na ufaulu wa 84.21% huku ikifanikiwa kupunguza idadi ya wanafunzi waliopata alama sifuri kutoka 1,477 mpaka kufika wanafunzi 608 tu.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo amethibitisha, halmashauri hiyo kuendelea kupata matokeo mazuri zaidi kwa kuendelea kushirikiana na Idara ya Elimu kufanya kazi kama timu huku akiwa na jukumu kubwa la kuwahimiza walimu kutekeleza majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kufundisha kwa bidii kwa kufuata miongozo pamoja na viwango vya upimaji wanafunzi vilivyowekwa na Udhibiti Ubora wa Elimu.
Licha ya kupata matokeo mazuri yaliyowezasha halmashauri ya Arusha kushika nafasi ya 21 kitaifa, Mkurugenzi huyo amezitaja changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa nyumba za walimu hasa kwenye maeneo ya vijijini jambo linalosababisha shule hizo kuwa na upungufu wa walimu pamoja na baadhi ya wanafunzi kushindwa kupata chakula cha mchana wawapo shuleni, kutokana na mwamko hafifu wa wazazi kuchangia chakula hicho.
Ameongeza kuwa, kutokana na ongezeko hilo la ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba mwaka huu, tayari halmashauri imekumbwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 109, ili wanafunzi hao kuweza kuanza masomo yao pindi watakapochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mapema Mwezi Januari mwaka 2019.
Aidha, Mkurugenzi Mahera anawataka wadau wote wa maendeleo kujitokeza, kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano kwa kuchangia ujenzi wa madarasa kwa shule za sekondari, ili wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza waweze kuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia.
Halmashauri ya Arusha ina jumla ya shule za msingi 138 kati ya hizo shule 46 ni za binafsi na shule 92 zinamilikiwa na serikali huku kukiwa na ongezeko kubwa la uandikishwaji wanafunzi kwa shule za serikali, kwa madarasa ya awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza, hii ni kutokana na serikali kutekeleza sera ya elimu bila malipo jambo linalosababisha upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa pamoja na madawati.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.