Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Seleman H. Msumi, amewataka walimu wakuu wa shule za sekondari kuongeza jitihada na mbinu bora za ufundishaji ili kuinua ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa.
Akizungumza katika kikao cha Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) kilichofanyika leo, Bw. Msumi alisema kuwa jukumu la msingi la viongozi wa shule ni kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora yenye tija kwa maisha yao na maendeleo ya taifa.
“Walimu wakuu ni nguzo muhimu katika kusimamia taaluma. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunaleta matokeo chanya kwa kuongeza nidhamu ya kitaaluma, kufuatilia kwa karibu ufundishaji na kutafuta mbinu mpya zitakazowezesha wanafunzi kuelewa masomo kwa urahisi zaidi,” alisema Bw. Msumi.
Aidha, aliwataka walimu wakuu kushirikiana kwa karibu na walimu walioko chini yao, pamoja na wazazi, ili kujenga mazingira bora ya kujifunzia yanayochochea ufaulu.
Kwa upande wao, viongozi wa TAHOSSA walimshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa ushauri na mwongozo wake, wakiahidi kuongeza juhudi za kuhakikisha ufaulu katika shule za sekondari za Wilaya ya Arusha unaimarika zaidi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.