Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema zinahitajika tafiti za kina pamoja mikakati katika kufanya mapinduzi ya kitamaduni kubadili tabia na mazoea yasioyafaa yanayojitokeza katika jamii hivi sasa ambayo ni kikwazo kwa maendeleo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Kusherehekea Miaka 30 ya Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) uliyofanyika katika Ukumbi wa Johari Rotana Jijini Dar es Salaam. Ametaja baadhi ya mazoea na tabia hizo ni pamoja na kutojali muda, kutokuwa na uaminifu mahali pa kazi pamoja na kutumia njia zisizofaa katika kupata kipato.
Makamu wa Rais ameitaka ESRF pamoja na Watalaam wa Fikra Tunduizi (Think Tank) kuangazia pia tabia za hivi karibuni za vijana kushiriki katika mahusiano na wanawake waliyowazidi umri maarufu (mashangazi) kama njia rahisi ya kujikimu, kutumia muda mwingi bila kufanya kazi kwa kushinda vijiweni, uchezaji kamari, utupaji taka ovyo, uchomaji moto ovyo wa nyasi na misitu pamoja na ubinafsi.
Pia Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuangazia tabia zingine kama vile matumizi makubwa ya fedha katika anasa kuliko kuweka akiba ikiwemo uchangiaji zaidi katika matukio ya sherehe na tafrija kuliko kusaidia gharama za elimu na matibabu kwa familia za kipato cha chini. Mengine ni kuongezeka kwa tabia ya utegemezi pamoja na kukithiri kwa vitendo vya ukatili kwa wanawake, watoto pamoja na vitendo vya ushirikina ikiwemo mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa rai kwa ESRF kufanya tafiti katika maeneo mengine muhimu ikiwemo hatari za kimataifa kama vile mabadiliko ya haraka ya Teknolojia, kutokuwa na uchumi stamihilivu, mizozo mikali inayopelekea mivutano ya kisiasa pamoja na kufanya tafiti kufahamu mienendo ya soko la ajira na namna vijana watakavyoweza kuendana nayo. Amesema ili kutumia vema idadi kubwa ya vijana iliyopo barani Afrika ikiwemo Tanzania, Taasisi za Tafiti zinapaswa kuanisha ufadhili endelevu wa miradi na programu zinazopendelewa na vijana kulingana na vipaumbele vya Taifa.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.