MKUU WA WILAYA YA ARUMERU APONGEZA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BWENI LA WANAFUNZI 80 SHULE YA SEKONDARI LOSINONI
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Amir Mohammed Mkalipa amepongeza jitihada za ujenzi wa bweni la wanafunzi 80 katika Shule ya Sekondari Losinoni, mradi ambao unalenga kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi wa eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ziara yake shuleni hapo, Mhe. Mkalipa alisema kuwa mradi huo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha sekta ya elimu kwa kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata mazingira bora ya kusomea na kujifunzia.
"Ujenzi wa bweni hili ni hatua kubwa katika kupunguza changamoto za wanafunzi hasa wale wanaotoka maeneo ya mbali. Hii itawapa fursa ya kusoma kwa utulivu na kuongeza ufaulu wao," alisema Mhe. Mkalipa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa shule hiyo, mradi huo unatarajiwa kugharimu kiasi cha Tsh. 163,252,633.93 hadi kukamilika kwake. Ujenzi umeanza kwa ushirikiano wa Serikali, Wananchi, na Wadau wa Maendeleo katika eneo hilo.
Aidha, Mkuu wa Wilaya alitoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya shule hiyo, akisema kuwa elimu ni msingi wa maendeleo na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha miradi mingine ya maendeleo katika sekta ya elimu inaendelezwa.
Shule ya Sekondari Losinoni inahudumia wanafunzi kutoka vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Arumeru, na kukamilika kwa bweni hili kunatarajiwa kupunguza changamoto za usafiri na kuboresha maisha ya wanafunzi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.