Na. Elinipa Lupembe.
Wajumbe wa Kamati ya Kupambana na ukatili wa kijinsia - MTAKUWWA halmashauri ya Arusha, wameiomba serikali, kuangalia namna ya kutekeleza sheria za kuwabana watu wanafanya ukatili kwa wanawake na watoto, kutokana na ukweli kwamba, jamii imeanza kubadilika na kutoa taarifa za matukio ya ukatili, lakini bado kesi zikikwama kutokana na baadhi ya sheria kukinzana.
Wajumbe hao, wameyasema hayo, wakati wa kikao kazi cha 'MTAKUWWA' cha kujadili taarifa za robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2021/2022, halmashauri ya Arusha, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa shirika la SOS- Children Ngaramtoni.
Akiwasilisha taarifa za shughuli za utekelezaji za MTAKUWWA, halmashauri ya Arusha kwa kipindi cha robo ya pili, Afisa Maendeleo ya Jamii anayesimamia Dawati la Jinsia, Lovil Nguyaine, amesema kuwa, licha ya kuwa bado changamoto ya ukatili wa kijinsia inaendelea kwenye jamii, kwa sasa jamii imeanza kupata ufahau kwa kutoa taarifa za matukio hayo kwenye sehemu husika ikiwa ni pamoja na polisi na baadhi ya kesi kufikishwa mahakamani.
Aidha Nguyaine ameweka wazi kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwezi mwezi Oktoba mpaka Desemba, jumla ya matukio 163 ya ukatili yameripotiwa na kufanyiwa kazi kupitia mamlaka mbalimbali za kisheria, huku matukio 6 yakiwa polisi na mengine yako Mahakamani kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.Hata hivyo, Afisa Jinsia huyo amethibitisha kuongezeka kwa matukio ya kutelekeza familia hata kufikia matukio 49 kwa kipindi cha miezi 3, hali ambayo inatishia maslahi na makuzi ya watoto, hivyo ni vema jamii ikaanza kuchukua tahadhari na sheria kuchukua mkondo pale mzazi atakapotelekeza familia.
Hata hivyo wajumbe hao, licha ya kukubaliana kuendelea kutoa elimu ya ukatilia kwa jamii, ili jamii iendelee kutoa ushirikiano hasa matukio hayo yanapofika kwenye vyombo vya usalama, polisi na mahakamani, lakini bado wameendelea kuzilalamikia sheria kinzani, zinazompa haki mtuhumiwa wa ukatili na kusababisha wanajamii kukata tamaa na kushindwa kuendelea na kesi.
Wameongeza kuwa, endapo watuhumiwa wanaofanya vitendo vya ukatili na kuripotiwa kituo cha polisi na kufikishwa mahakamani, kesi hizo zikishughulikiwa kwa haki na kuwatia hatiani watuhumiwa hao, itasaidia kutokomeza ukatili dhidi ya watoto na wanawake katika jamii zetu.
"Inakatisha tamaa sana, mtoto amefanyiwa vitendo vya ukatili, amebakwa na mtoto anakiri kubakwa na kumtaja aliyemfanyia hivyo, lakini sheria bado inamlinda mbakaji, na wakati mwingine kumuachia huru, kwa vigezo ushahidi unaonesha hana hatia, hali hii inarusdisha nyuma harakati za kutokomeza ukatili kwenye jamii zetu" Wamesema wajumbe hao.
Awali Kamati ya Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto MTAKUWWA, halmashauri ya Arusha, kwa kushirikiana na wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali, inaendelea kutekeleza wajibu wake, kwa kupamba na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto huku mafanikio ya kamati hiyo yakiendela kuzaa matunda ndani ya jamii.
ARUSHA DC
KaziInaendelea✍✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.