Na Elinipa Lupembe
Hatimaye mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa kijiji cha Losinoni Kati kata ya Oldonyowas na mwekezaji wa shamba la Korfovoun Estate Ltd, umefikia kikomo baada ya mwekezaji huyo kuridhia kutoa sehemu ya shamba lake ekari 222 kati ya Eka 700 na kuwakabidhi wananchi wa kijiji hicho.
Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 20, umefikia muafaka kwa mazungumzo na maridhiano baina ya mwekezaji na viongozi wa kijiji yaliyoongozwa na mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuella Mtatifikolo Kaganda na Kamati ya Usalama wilaya.
Akizungumza wakati wa kuoneshana mipaka ya maeneo hayo, mmiliki wa shamba hilo Bw. Robert Daniel, amesema kuwa amekabidhi eneo la Eka 222, kwa kuzichanganua Eka 116 kwa serikali ya kijiji, Eka 23 kwa shule ya msingi Engedeko, Eka 11 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari na Eka 71 kwa wananchi ambao tayari walivamia na kujenga makazi yao.
"Eneo la shamba lililobaki tunatarajia kuanza kilimo cha pareto na mazao mengine hivyo ninaomba wananchi kushirikiana nami, katika shughuli hizo, kampuni itatoa ajira kwa wazawa wakati wote wa kutekeleza mradi wetu" Amesema Robert
Naye Mkuu wa wilaya ya Arumeru, mara baada ya kuoneshwa mipaka ya maeneo hayo, amemuagiza mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Seleman Msumi kupitia Idara ya Ardhi, kuanza mchakato wa kuandaa kutenganisha hati ya shamba la mwekezaji na maeneo aliyoyatoa, kuweka mipaka maeneo yote yaliyotolewa kwa Umma, taasisi pamoja na kuwasaidia wananchi kurasimisha na kupima maeneo yao ili wapate hati miliki.
"Leo tumeoneshwa mipaka ya maeneo aliyoyatoa mwekezaji kwa kijiji, shule na wananchi ambao tayari mlijenga kwenye shamba lake, ninakuagiza Mkurugeni na Idara ya Ardhi, zoezi hili lisichukue muda mrefu, maeneo yaliyotolewa kwa shule yawekewe 'bicon' na kuyapima, wananchi wasaidieni kurasimisha na kuyapima waweze kupata hati miliki, ili mgogoro huu usijirudie tena" Amesema Mhe. Emmanuella.
Hata hivyo amewaagiza viongozi wa kijiji na vitongoji kuwaelimisha wananchi wao juu ya umiliki halali wa mwekezaji wa shamba hilo pamoja na kuheshimu mipaka ya shamba lake, kwa kuzingatia kuwa mwekezaji amewagawia maeneo kutoka sehemu ya shamba lake bure na zaidi hata wananchi waliovamia na kujenga ndani ya shamba ameridhia kuwaachia na kuruhusu wapimiwe na kumilikishwa kisheria.
Aidha amewasisitiza viongozi hao, kutoa ushirikiano kwa watalamu wa ardhi wakati wote watakapofika kijijini hapo kupima na kuweka mipaka maeneo hayo ili kurahisisha zoezi hilo liende kwa haraka na kukamilika kwa wakati.
Hata hivyo wananchi wa kijiji cha Losinoni kati wameishukuru serikali kwa kusimamia na utatuzi wa mgogoro huo wa muda mrefu ambao wamekiri ulikwamisha shughuli nyingi na kuchelewesha maendeleo yao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Losinoni Kati Mhe. Peter Gabriel amemshukuru Mkuu wa wilaya na mwekezaji kwa kukubali kutoa sehemu ya eneo la shamba lake na kuwagawia wananchi na kijiji pia.
Ametupa eneo la shule ya msingi Eka 22, Eka 11 kwa ajili ya kujenga shule ya sekondari, lakini pia amerasimisha Eka 71 ambazo wananchi walivamia na kujenga, na Eka 116 kwa ajili ya kijiji chetu, tunamshukuru sana na nitawasimamia wananchi kumpa ushirikiano katika shughuli zake kilimo anazotarajia kuzifanya kijijini hapa" Amebainisha Mwenyekiti.
PICHA ZA MATUKIO
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.