Na Elinipa Lupembe
Kufuatia mkakati wa Serikali wa kuwa na shule ya sekondari kila kata, kupitia program ya kuboresha miundo mbinu ya elimu kwa shule za sekondai (SEQUIP) imetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 584.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Moivo.
Akizungumza na ofisini kwake na mwandishi wa habari hizo, mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Seleman Msumi amekiri kiasi hicho cha fedha kimepokelewa kwenye akaunti ya shule mama ya Sekondari Enyoito na tayari mchakato wa ujenzi umeanza.
Ameweka wazi kuwa kiasi hicho cha fedha kitatumika kujenga vyumba 8 vya madarasa, maabara 3 za masomo ya Sayansi, chumba cha masomo ya TEHAMA, matundu 8 ya vyoo yenye sehemu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na chumba maalum cha kubadilishia wasichana.
"Kama ilivyo utaratibu wa serikali, ujenzi utatekelezwa kupitia 'force akaunti' huku shughuli zote zikifanyika kwenye ngazi ya jamii kwa usimamizi wa watalaam wa ofisi yangu". Amefafanua Mkurugenzi Msumi
Hata hivyo Msumi, amemshukuru Mheshimiwa Rais na kuipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kasi ya kuboresha sekta nyeti ya elimu, na kuongeza kuwa fedha zimekuja wakati muafaka kwa kuwa kata ya Moivo ina idadi kubwa ya watoto ambao wanasoma shule za kata jirani za Ilkiding'a na Enyoito, jambo ambalo linasababisha msongamano wa wanafunzi kati shule hizo.
Naye Afisa Elimu Sekondari, Mwl. Menard Lupenza amethibitisha umuhimu wa shule hiyo, licha ya kuwa na shule kata ya Moivo lakini utaondoa msongamano wa wanafunzi kwa shule za jirani na kurahisisha tendo la kujifunza na kufundishaji kwa walimu na wanafunzi pamoja na kupandisha kiwango cha taaluma shuleni hapo.
"Kutokana na serikali kutoa elimu bila malipo kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari, hivyo kuna uhitaji mkubwa wa shule za sekondari kwa kila kata"Ameweka wazi Afisa Elimu huyo
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa shule hiyo mpya ni utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020 -25 Sura ya Tatu, Ibara ya 79 (i) Kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya sekondari kwa: kuongeza idadi ya shule za sekondari.
ARUSHA DC NI YETU, TUSHIRIKIANE KUIJENGA,
#KaziIendelee
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.