Wanafunzi na wanamichezo wanaoshiriki michezo ya shule za sekondari 'UMISETA', halmashauri ya Arusha, wametakiwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika michezo hiyo, jambo ambalo litawapeleka kwenye mafanikio ya ushindi.
Rai hiyi imetolewa na Mkurugenzi mtendaji, halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera, wakati wa uzinduzi wa Bonanza la UMISETA lililofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Ilboru mwishoni mwa wiki iliyopita.
Dkt. Mahera amewataka wanafunzi hao kuwa nidhamu wakati wote wa mashindano hayo, kwa kuwa nidhamu ndio msingi mkuu, si kwa michezo tuu hata katika taaluma pia.
Ameongeza kuwa nidhamu ndio nguzo ya mafanikio kwaa mtu yoyote, na kufafanua kuwa, watu wengi waliofanikiwa ni wenye nidhamu, kuanzia nyumbani, kwa jamii, shuleni mpaka katika kutekeleza majukumu yao wawapo kazini.
"Mwanafunzi mwenye nidhamu anayo nafasi kubwa sana ya kufanya vizuri kitaaluma, pamoja na kufika mbali kwa kupata mafanikio hata ya kimaisha" amesema Dkt.
Aidha Dkt. Mahera amefafanua kuwa, michezo ni afya ya kufanya mwili kuwa 'active' na kuifanya akili kuweza kufanya kazi kwa weledi pamoja na kuleta upendo, kufahamiana na kushirikiana.
Hata hivyo mkurugenzi huyo, amewataka walimu na makocha kuunda timu mahiri zenye wachezaji wanaojituma katika mashindano hayo ili kupata ushindi kuanzia ngazi ya mkoa mpaka taifa.
Naye Afisa Utamaduni na Michezo, halmashauri ya Arusha, mwalimu Gasper Tesha, amesema kuwa Bonanza hilo linafanyika kwa kushindanisha timu kutoka kanda 5 za halmashauri hiyo kwa lengo la kuchakua na kupata wachezaji bora watakaounda timu zitakazowakilisha halmashauri kimkoa kuanzia tarehe 26.05.2018.
Tesha ametaja michezo itakayoshirikishwa ni pamoja na soka la wavulana na wasichana, mpira wa pete, kikapu, wavu,meza,riadha, bao na michezo ya sanaa na maonesho.
Hata hivyo Tesha ameongeza kuwa, Bonanza hilo limeshirikisha jumla ya wanafunzi 120 wakike na kiume, lakini watachujwa na kubaki wanafunzi 90 ambao wataunda timu za michezo yote na kuwakilisha halmashauri kimkoa.
Rahma Saida mwanafunzi wa shule ya sekondari Oldadai, na mchezaji kutoka kanda ya Sokoni II, ameahidi kufanya vizuri katika mashindano hayo na amewataka wazazi kuwaandaa watoto wakike kujitambua ili wawaruhusu kushiriki michezo kwa kuwa wazazi wengi, huwazuia watoto wao wa kike kushiriki michezo kwa kuhofia kujiingiza kwenye vitendo vibaya.
Naye Amir Waziri wa Kanda ya Ilboru amesema kuwa wamejipanga kufanya vizuri kwenye mashindano hayo mpaka ngazi ya taifa licha ya changamoto za ukosefu wa viwanja vya michezo vyenye viwango kwenye shule zao.
Kanda zitakazoshiriki Bonanza hilo ni pamoja na kanda ya Sokoni II, Ilboru, Kisongo, Mlangarini na Kiranyi ambazo zimtoa wachezaji kutoka shule za sekondari katika maeneo hayo.
Michezo ya UMISETA kitaifa yanatarajiwa kufanyika kitaifa mkoani Mwanza yenye kauli mbiu ya 'Michezo, Sanaa, Taaluma ndiyo Msingi wa Maendeleo'.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.