Na. Elinipa Lupembe
Umoja wa nchi zinazouza mafuta Duniani OPEC, unaofadhili miradi ya kunusuru kaya masikini, miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii - TASAF, umeridhishwa na utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa katika halmashauri ya Arusha wilaya ya Arumeru, miradi inayoonyesha dhahiri, matunda ya kupambana na umaskini kwa jamii na kuahidi kuendelea kufadhili miradi hiyo nchini Tanzania.
Akizungumza wakati alipotembelea na kukagua Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule mpya ya sekondari Oldonyowas, mapema wiki hii, mmoja wa maafisa waandamizi wa OPEC, Sharagim Shams amekiri wazi kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo ya TASAF, na kusema kuwa, ameona miradi hiyo ni ya kiwango kizuri kinachoridhisha, hali inayosababisha Umoja huo, kukubali kuendelea kufadhili miradi ya kupunguza umaskini nchini, hasa katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa manufaa ya watanzania na vizazi vijavyo.
‘’Nimevutiwa sana utekelezaji wa miradi tunayoifadhili sisinkama OPEC, na nimeshuhudia namna ambavyo imetekelezwa kwa ubora mzuri, ubora unaoonekana kuwanufaisha wananchi masikini ambao wamekusudiwa na mradi, nimefurahishwa zaidi na ushiriki wa wananchi katika miradi, hivyo tutaendelea kufanyakazi na serikali ya Tanzania kupitia TASAF’’ amesisitiza Sharagim Shams.
Aidha Shams amewashauri walengwa wa TASAF na wananchi wengine kutumia vizuri fursa ya miradi hiyo, kuondokana na umasikini uliokithiri, pamoja na kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule kupata elimu, hususani kwenye shule zinazojengwa na TASAF kwa ufadhili wa OPEC ili kujenga raslimali watu iliyoelimika kwa siku zijazo.
Wakitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa ujumbe wa wataalamu kutoka OPEC, Wizara ya Fedha na TASAF, wakazi wa kijiji cha Oldonyowas, ambao wamenufaika na miradi hiyo, wamesema kuwa, ujenzi wa miradi hiyo katika eneo lao, umeleta mapinduzi makubwa ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na hamasa kubwa ya kupambana na umaskini uliokithiri, sambamba na kuwahamasisha wananchi wajamii ya wafugaji kuwapeleka watoto wao shule, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Wananchi wa kata ya Oldonyowas, wamekiri watoto wao kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu, wa kwenda kufuata shule za sekondari kata nyingine, jambo lililosababisha watoto wengi kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo, huku watoto wengi wakishindwa kumaliza elimu hiyo, wasichana waiishia kuolewa katika umri mdogo na kukatisha ndoto za maisha yao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyowas, mheshimiwa Geophray Ayao, amethibitisha kuwa, ujenzi wa shule hiyo ya Oldonyowas umeleta mwanga kwa wazazi na watoto wao na kuwa wana imani sasa watoto wao watafanya vizuri katika masomo na hatimaye kutimiza ndoto zao, na kuwa na vijana wasomi katika kata yao.
"Awali watoto walikuwa wanakwenda shule ya sekondari Oldonyosambu, shule ambayo ipo umbali wa zaidi ya Kilomita 12, umbali ambao uliwakatisha tamaa watoto wengi, na kushindwa kufaulu masomo yao na wengine kushindwa kuendelea na masomo na kuacha shule kutokana na umbali huo, jambo ambalo kwa sasa litakuwa historia, katika kijiji chetu" amefafanua Mwenyekitu huyo wa kijiji.
Hata hivyo, kupitia utaratibu wa ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kuwashirikisha wananchi, Serikali kupitia TASAF kwa ufadhili wa OPEC, imeweza kutatua tatizo lililokuwa linawakabili wakazi wa kijiji cha Oldonyowas la ukosefu wa shule ya sekondari na uhaba wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, mabweni ya wanafunzi pamoja na matundu ya vyoo katika shule ya sekondari kijijini hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Tanzania, Ladislaus Mwamanga, amewapongeza wananchi wa kijiji cha Oldonyowas kwa namna walivyoitikia mwito wa serikali wa kushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo, jambo ambalo amekiri, limesaidia kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na ufanisi mkubwa.
Mwamanga pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuruhusu utekelezaji wa sehemu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF, hatua ambayo amethibitisha inatoa mchango muhimu katika mapambano dhidi ya umaskini ikiwa ni utekelezaji wa Ilani Chama cha Mapinduzi kama ilivyonadiwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 inavyoelekeza.
Akitoa shukrani zake kwa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF ) mkuu wa shule ya sekondari Odonyowas Richard Mugyabuso, licha ya kuushukuru umoja wa OPEC kupitia Serikali, amefafanua kuwa TASAF imejenga miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa, jengo la utawala ,mtundu ya vyoo manne pamoja na ujenzi wa mabweni mawili unaoendelea shuleni hapi kwa ajili ya wanafunzi 96 wa kike.
Pia mwalimu huyo ameeleza kuwa licha ya mafanikio hayo makubwa bado shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wa ukosefu wa mabweni,upungufu wa vyumba vya madarasa unaoendana na uwiano wa idadi ya wanafunzi waliodahiliwa shuleni hapo pamoja na tatizo la maji na kuiomba OPEC kupitia TASAF kuendelea kufadhili shule hiyo ili kuwezesha wanafunzi kujifunza katika mazingira bora zaidi.
“Ninaimani kabisa changamoto hizi zikitatuliwa itasaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi shuleni hapa kwani kwa sasa hivi bado kuna wanafunzi wanatoka umbali mrefu huku wengine wakitembea umbali wa hadi Kilometa 12 kuja shuleni, hivyo mwanafunzi anafika shuleni amechoka na jambo linalimpotezea utulivu wa kumsikiliza mwalimu anapokuwa akifundisha, uwepo wa mabweni yakutosheleza utatusaidia watoto kufanya vizuri katika masomo yao“ alibainisha mugabuso .
Naye Mratibu wa TASAF halmashauri ya Arusha Grace Makema ameeleza kuwa, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF kwa ufadhili wa OPEC kupitia miradi ya Mpango wa Kunusu Kaya Masikini, umetekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule ya sekondari Oldonyowas, miradi iliyoibiliwa na wananchi wenyewe, kwa na gharama ya shilingi milioni 436.3, na kuchanganua gharama hizo kuwa ni ujenzi wa jengo la utwala milioni 104.5, vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na matundu mnne ya vyoo milioni 79.8, nyumba ya walimu yenye sehemu mbili (2 in 1) milioni 76.9, mabweni mawili kwa milioni 175.1, TASAF ikitoa shilingi milioni 384 huku jamii ikichangia kiasi cha shilingi milioni 52.2 sawa na asilimia 12.
Miradi inayofadhiliwa na OPEC kupitia TASAF inatekelezwa katika mikoa ya Njombe na Arusha Miradi kama hiyo imekwishatekelezwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara nakiwa na lengo kuuu la kusaidia jitihada za wananchi na serikali kutatua changamoto za maendeleo ya wananchi na miradi ambayo huibuliwa na wananchi wenyewe.
PICHA ZA MATUKIO
Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, mhe. Baraka Simon akimkabidhi zawadi mwakilishi kutoka Umoja wa nchi zinazouza Mafuta Duniani,Sharagim Shams, wakati alipotembelea na kukagua miradi ya TASAF shule ya sekondari Oldonyowas.
Mratibu wa TASAF halmashauri ya Arusha, Grace Makema akimkabidhi zawadi mwakilishi kutoka Umoja wa nchi zinazouza Mafuta Duniani,Sharagim Shams, wakati alipotembelea na kukagua miradi ya TASAF shule ya sekondari Oldonyowas.
Muonekano wa majengo ya shule ya sekondari ya Oldonyowas
Jengo la Utawala shule ya sekondari Oldonyowas
Bweni la wasichana shule ya sekondari Oldonyowas.
Ugeni kutoka OPEC wakikagua nyumba ya walimu, shule ya sekondari Oldonyowas
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.