Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella, amemuagiza mkuu wa wilaya ya Arumeru, kupitia mkurugenzi mtendaji, halmashauri ya Arusha, kuongeza kasi ya kusimamia ukamilishaji wa jengo la zahanati ya Kigongoni kata ya Bwawani, jengo ambalo limejengwa kwa muda mrefu sasa.
Mhe. Mongela amesema kuwa, jengo hilo la Zahanati ni muhimu kwa wananchi wa kijiji cha Kigongoni, hivyo ameagiza kuongeza kasi ya usimamizi wa ukamilisha wa jengo hilo na kusisitiza kuwa ifikapo Novemba 2023, zahanati hiyo iwe imekamilika na kufunguliwa ili wananchi waanze kupata huduma za afya kituoni hapo.
"DC na mkurugenzi kamilisheni jengo hili, licha ya kutoa huduma za afya kwa wananchi hawa, lakini inawapa ari na nguvu wananchi kuendelea kuchangia utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao, tuwatie moyo wananchi kuchangia maendeleo katika maeneo yao" Amesisitiza kwa hisia kali RC Mongela
Awali Zahanati hiyo ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi na kufikia lenta kwa gharama ya shilingi milioni 25, na baadaye halmashauri ilitoa milioni 60 kwa awamu mbili za mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 huku mwaka huu wa fedha 2023/24, ikitengewa shilingi milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo, tayari kwa kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha katika mradi huo, Mhe. Mongellaa amewaagiza na kuwasisitiza wahandisi, kuwacha kutumia mbao za mti wa Mloliondo licha ya kuwa ni mbao ngumu, lakini mbao hizo hazidumu, huharibika haraka kutokana na kushambuliwa na wadudu, badala yake kutumia mbao ambazo hudumu kwa muda mrefu licha ya kuwa zina gharama kubwa.
Awali mkuu huyo wa mkoa katika siku ya pili ya ziara yake, amekagua utekelezaji wa zahanati na mradi wa umeme REA kijiji cha Kigongoni, ujenzi wa kituo kipya cha afya kata ya Bwawani pamoja na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kata hiyo.
ARUSHA DC NI YETU, TUSHIRIKIANE KUIJENGA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.