Na. Elinipa Lupembe.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Idd Kimanta amewataka watumishi wa halmashauri ya Arusha kusimamia fedha zinazoletwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa ameyasema hayo, wakati alipofanya kikao kazi na watumishi wa halmashauri ya Arusha, mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni kikao chake cha kwanza na watumishi wa halmashuri hiyo tangu alipoteuliwa na mheshimiwa Rais, kikao kilichofanyika kwenye, ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Amesema kuwa, Serikali imekuwa ikileta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo ni jukumu la watendaji wote wa serikali, kuisimamia miradi hiyo kwa weledi pamoja na kusimamia matumizi sahihi ya fedha za miradi hiyo, kwa kuzingatia kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za Umma.
“Simamieni utekelezaji wa miradi, simamieni matumizi ya fedha zote za miradi ya maendeleo, hakikisheni miradi hiyo inatekelezeka kwa wakati na kukamilika ikiwa na ulinganifu wa ubora na thamani ya fedha kwa mmaendeleo ya wananchi katika maeneo yenu”. Amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa amani, upendo na kwa kushirikiana, kwa kuwa kila mmoja ana mchango wa kumuinua mwenzake katika utumishi wa Umma.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule, amekiri kupokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi hasa katika usimamizi wa miradi yote ya maendeleo kwa manufaa ya Umma.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa, watumishi wa halmashauri hiyo, wako tayari kutekeleza majukumu yao, kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa Umma, na kuongeza kuwa atawasimamia stahiki za watumishi hao, ili waelekeze nguvu zao katika kuwatumikia wananchi.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wote, Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Arusha, Angela Mvaa amesema, wamefarijika sana kupokea maelekezo, kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, maelekezo yaliyojaa hekima na busara nyingi, na wapo tayari kuyafanyia kazi, kwa maslahi ya wananchi wa halmshauri hiyo na taifa kwa ujumla.
Awali Mkuu huyo wa Mkoa amekutana na kuzungumza na watumishi hao, lengo likiwa kufahamiana na kupeana maelekezo ya namna ya kutekeleza majukumu yao katika utumishi wao wa Umma.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.