Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella amekagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi kijiji cha Lemanda kata ya Oldonyosambu.
Mradi huo umetekelezwa na serikali kwa gharama ya shilingi milioni 306.9 fedha kutoka serikali kuu kupitia mradi wa Kuboresha Upatikanaji wa Fursa sawa katika Ujifunzaji Bora kwa Elimu ya Awali na Msingi Tanzania Bara (BOOST).
Mradi huo ukiwa tayari umekamilika kwa zaidi ya asilimia 95, huku Mkuu huyo wa mkoa akiuagiza uongozi wa wilaya kupitia halmashauri, kuharakisha taratibu za usajili shule hiyo ili watoto waanze kusoma shuleni hapo na kufaidi matunda ya serikali yao makini.
Hata hivyo amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Arumeru, kutoa fedha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kukamilisha jengo lenye vyumba vya madarasa ambalo lilijengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji cha Lemanda, jengo ambalo linahita kiasi cha shilingi milioni 15 huku akiwata wananchi kutoa shilingi milioni 5 wakiongozwa na Mhe. Diwani wa kaya ya Oldonyosambu kwa kushirikiana na mwenyekiti wa kijiji cha Lemanda
"Majengo yote yanavutia na yanapendeza sana, hili moja linatia doa, DC na Mkurugenzi, jipangeni kupitia mapato ya ndani wajazieni nguvu wananchi hiyo milioni 10 ili jengo hilo liweze kukamilika, wanafunzi wakianza shule wakute majengo yote ni mapya" Amesisitiza Mhe. Mongella
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Oldonyosambu Mwl. Hoza, amebainidha kuwa kiasi hicho cha fedha kimejumuisha ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa ya shule ya msingi, vyumba 2 vya madatasa ya shule ya awali ya mfano, jengo la utawala pamoja na matundu 20 ya vyoo.
Hata hivyo Diwani wa kata ya Oldonuosambu, Mhe. Raymond Lairumbe kwa niaba ya wananchi, hakusita kuishukuru serikali ya awamu ya sita na uongozi wa mama Samia Suluhu kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza mradi mkubwa ambao kwao ilikuwa ni ndoto.
"Naweza kusema Mhe. Rais ametufanyia 'suprise' kubwa ambayo ilikuwa ni ndoto yetu ya muda mrefu, ndoto ambayo hatukujua ufumbuzi wake, lakini serikali ya awamu ya sita imetufanyia kweli kwa kipindi kifupi ambacho hatukutarajia, tunamuombea kwa Mungu aendele kumjalia afya njema achape kazi ya kuwatumikia wananchi hasa waishio vijiji vya mbali kama hiki cha Lemanda" Amesisitiza Mhe. Lairumbe
Ameongeza kuwa, kulikuwa na uhitaji mkubwa wa shule hiyo, kutokana na watoto wa kijiji hicho kutembea umbali wa zaidi ya Km 10 kwenda kusoma shule ya msingi Oldonuosambu, jambo ambalo licha ya watoto kuteseka lakini lilisababisha watoto kuanza shule kwa kuchelewa huku baadhi ya watoto kushindwa kusoma kabisa.
Awali Mkuu huyo wa mkoa, anafanya ziara ya siku mbili 19 & 20. 09.2023 ya kukagaua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya Elimu sekondari na Msingi, miundombinu ya barabara na maji, pamoja na kufanya mikutano ya hadhara na kusikiliza kero za wananchi katika kata za Oldonyowas na Bwawani.
Arusha DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.